Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 3962151.UZINDUZI WA JUKWAA LA UCHUMI WA KIJANI

HOTUBA  YA  MHESHIMIWA  DKT.  MOHAMMED GHARIB  BILAL,  MAKAMU  WA  RAIS  WA JAMHURI  YA  MUUNGANO  WA  TANZANIA KATIKA  UZINDUZI  WA  JUKWAA  LA  UCHUMI WA  KIJANI  
MJINI  IRINGA TAREHE  08  MEI, 2012

 

veysel karani hz mehdi recent business newsmagazine newsfirst class business all places haber cook recipe


 

HOTUBA  YA  MHESHIMIWA  DKT.  MOHAMMED GHARIB  BILAL,  MAKAMU  WA  RAIS  WA JAMHURI  YA  MUUNGANO  WA  TANZANIA KATIKA  UZINDUZI  WA  JUKWAA  LA  UCHUMI WA  KIJANI  
MJINI  IRINGA TAREHE  08  MEI, 2012
 
 
 
 
Mhe. Christine Gabriel Ishengoma
Mkuu wa Mkoa;
 
Mhe. Adam Malima
Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika;
 
Mhe. Balozi wa Finland;
 
Mhe. Mchungaji Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini;
 
Waheshimiwa Wabunge Mliopo;
 
Viongozi wa Dini;
 
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
 
Wageni Waalikwa;
 
Mabibi na Mabwana.
 
Kwanza kabisa naomba nianze kwa kuwashukuru viongozi wa Taasisi ya Uongozi wa Jukwaa la Uchumi wa Kijani kwa kunialika leo hapa kwa kazi hii ya kuzindua Jukwaa hili la Uchumi wa Kijani. Napenda kuchukua fursa hii pia kuwashukuru waandaaji wa jukwaa hili; kwanza kwa kubuni wazo la Jukwaa la Uchumi wa Kijani na pia kwa kuniomba kuwa mlezi wake, ombi ambalo nililikubali. Namshukuru pia Mkuu wa Mkoa na viongozi wote wa mkoa pamoja na wananchi wa Iringa kwa kutukaribisha vizuri, mimi binafsi pamoja na msafara wangu.  
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Tuko hapa leo kwa ajili ya uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi wa Kijani. Lengo la Jukwaa hili ni kuongeza uelewa wa watunga sera, watoa maamuzi na watu wenye ushawishi katika jamii kuhusu masuala yanayohusu uchumi wa kijani. Nimearifiwa kwamba Jukwaa hili la kwanza litajielekeza katika uchumi wa misitu na litafanyika hapa Iringa kwa kuwa mkoa huu ni mfano mzuri nchini katika masuala ya fursa za kiuchumi zitokanazo na misitu.
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Uchumi wa kijani ni uboreshaji wa uchumi na ustawi wa jamii unaozingatia uzalishaji na matumizi yasiyoharibu mazingira. Wengine hufikiria uchumi na mazingira kama masuala mawili tofauti ambayo harakati za kuyafikia malengo ya suala moja huathiri vibaya uwezekano wa kufanikisha malengo ya suala jengine. Uchumi wa Kijani huondoa uhusiano huu kinzani. Uchumi wa Kijani unahimiza mabadiliko ya mifumo ili kutambua kuwa ingawa uchumi na mazingira ni mahitaji ya kimaumbile kwa maisha ya binadamu, yanaweza kufikiwa sambamba.
 
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Ukuaji wa uchumi unaozingatia matumizi yasiyo endelevu ya maliasili hauna manufaa katika dunia ya leo. Watu wanapaswa kuachana nambinu zakizamaniza ukuaji wa uchumi wa matumizi shinikizi ya rasilimali, ambapo maendeleo yamekuwa yakigharimu mazingira; badala yake, wanapaswa kufuata mbinu mpya ambazo tija huongezwa kwa kutumia na kusimamia maliasili kwa ufanisi zaidi.
 
Aidha, shughuli za kiuchumi lazima zizingatie athari za muda mrefu kwa mazingira na haja ya kuhifadhi urithi wetu wa pamoja kwa faida ya vizazi vijavyo. Uchumi wa kijani huchochea ukuaji wa uchumi, mapato, na ajira. Tena husaidia kuimarisha mazingira na kuongeza tija kwa wananchi. Aidha aina hii ya uchumi huleta maendeleo ya kiuchumi ya muda mrefu na yanayotoa fursa kwa watu wengi.
 
Katika baadhi ya sekta muhimu kama vile kilimo, ujenzi, misitu, na usafiri, uchumi wa kijani hutengeneza ajira nyingi zaidi kuliko ambazo zipo katika hali ya kawaida. Katika sekta kama vile uvuvi; uchumi wa kijani utalazimisha kushuka kwa mapato na ajira katika muda mfupi na wa kati ili kujazia hifadhi asilia, lakini hali hii hubakia ya muda mfupi na baadaye sekta hukua na kutoa tija kubwa kwa wananchi.
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Jitihada za maendeleo nchini Tanzania lazima zifanywe kwa kuzingatia uhalisia wa mambo. Kwanza, zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa nchi hii huishi vijijini. Hivyo, jitihada madhubuti za kupunguza umaskini na kuleta maendeleo lazima zilenge wakazi na uchumi wa vijijini ili kuwa na matokeo mazuri.
 
Kuna uhusiano mkubwa kati ya watu maskini hasa wa vijijini na mazingira. Wao huishi karibu na mazingira ya asili na hutegemea rasilimali za ardhi, maji, na misitu kwa maisha yao.
 
Pia, kuzorota kwa mazingira ya asili kuna athari za moja kwa moja na za haraka katika kuporomoka kwa hali na ustawi wa maisha yao. Hivyo, bayoanuai si suala la kufikirika kisayansi tu kwa Watanzania, bali ni msingi wa maisha na ustawi wa binadamu. Kuhifadhi maliasili katika maeneo ambayo jamii maskini huishi ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu.
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Katika maeneo yetu mengi ya vijijini, mazingira yameendelea kuingiliwa na matumizi shindani ya rasilimali kwa maslahi ya kibiashara. Mara nyingi matumizi hayo yamezisababishia hasara jamii ikiwa ni pamoja na upotevu wa maisha na kipato. Mifano ya hasara hizo ni pamoja na jamii kupoteza misitu yao kutokana na upasuaji wa mbao; kupungua mazalia ya samaki na upungufu wa vyanzo vya maji.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, dhana za maendeleo endelevu na uchumi wa kijani zinapaswa kujumuisha haki za jamii za vijijini kusafisha mazingira yanayowawezesha kuwa na msingi madhubuti wa kuendesha maisha na ustawi wao. Maendeleo endelevu na mikakati ya uchumi wa kijani inapaswa kuweka kipaumbele katika sera na miradi inayozinufaisha jamii za vijijini.
 
Hapa hujumuisha kupiga marufuku shughuli zinazoharibu mazingira na vyanzo vya mapato ya jamii; urejeshaji wa mifumo ya ikolojia iliyoharibiwa; misaada ya shughuli endelevu za kilimo; uwekezaji katika mipango ya nishati jadidifu, maji, na usafi wa mazingira. Halikadhalika, suala la elimu na huduma bora za afya lazima vipewe msisitizo.
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Ingawa nimeweka msisitizo zaidi vijijini, masuala ya mazingira mijini ni muhimu kuzingatiwa. Maeneo ya miji hukabiliwa na changamoto za ubadilishaji wa matumizi ya ardhi kunakoendana na ukataji miti, uchimbaji mawe na pia ukaushaji wa ardhioevu, Haya na mengine mengi husababisha uharibifu wa mazingira na huchangia kwa kiwango kikubwa katika mabadiliko ya tabia nchi.
 
Vile vile, suala la uchafuzi wa hewa katika miji huleta madhara makubwa kwa afya ya wakazi pamoja na uoto na ardhi. Usafiri mijini huchangia uchafuzi wa hewa, na idadi kubwa ya magari na viwanda mijini huchangia sehemu kubwa ya uzalishaji wa gesi chafu mijini.
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Ukuaji wa miji nchini Tanzania haujasimamiwa vizuri katika maeneo yetu mengi yanayokua kwa kasi, hivyo kusababisha matatizo makubwa ya kimazingira na kiafya. Usimamizi bora wa mazingira mijini unaweza kusaidia kuepusha athari hasi nyingi za kimazingira, hivyo, sera za mipangomiji zinapaswa kuwa sehemu muhimu ya sera za kiuchumi. Ukuaji wa miji utaendelea kuwa ni sehemu muhimu kwa mazingira, uchumi, na maisha ya watu. Tunaelewa kuwa hivi sasa watanzania wengi zaidi wanaishi vijijini, lakini miaka michache ijayo hali hiyo itabadilika na watanzania wengi zaidi wataishi mijini. Kwa maana hiyo miji mipya itaibuka na iliopo itafurika watu. Changamoto iliyopo ni kujifunza jinsi ya kwenda sambamba na ukuaji huo huku tukitumia zaidi fursa na faida zake na kudhibiti madhara.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Tanzania inahitaji kuendelea, lakini inazidi kubainika kuwa kuendesha mambo kwa mazoea si chaguo sahihi tena. Mbinu mpya za ukuaji wa uchumi ni muhimu. Tunahitaji kutafuta njia za kuunganisha uendelevu wa mazingira, ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na kufanya mapinduzi ya ukuaji wa uchumi na jamii kwa kuachana na utumiaji hasi wa kupindukia wa mazingira unaosababisha ukosefu wa usawa na haki za kijamii.
 
Ajira bora, matumizi na uzalishaji endelevu bila kuathiri mazingira pamoja na mikakati ya tabianchi ya uzalishaji wa kiwango cha chini cha hewa chafu, ni masuala yanayoweza kuonekana kama njia ya kupatanisha mahitaji ya ukuaji wa uchumi na ongezeko la upungufu wa maliasili. Kama tujuavyo, hali hii itahitaji mabadiliko makubwa ya mifumo ya kijamii na kiuchumi.
 
Uchumi wa kijani unahitaji mabadiliko ya haraka ya tabia na mitazamo wa jamii. Changamoto kubwa inabaki kuwa kazi ya kuielimisha jamii juu ya athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya kiuchumi ni ngumu na inahitaji ufuatiliaji wa karibu. Sote kwa umoja wetu tunahitajika kufanya kazi hii pasipo kuchoka.
 
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Kama taifa tunazo changamoto nyingi za kimazingira. Mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani sambamba na uhaba wa wataalam wa kutosha ni mambo tunayotakiwa kuyapatia msisitizo. Lazima tukubali kubadilisha aina ya maisha tunayoishi na kuhamasisha wananchi juu ya kuziasili teknolojia mpya hasa zinazosisitiza matumizi ya nishati zisizoathiri mazingira katika shughuli za kila siku katika maisha yetu. Kwa upande wake Serikali yetu imejiandaa kupanua matumizi ya gesi asili kwa kupikia na matumizi mengine ili tupunguze uzalishaji wa gesi mkaa kwa kiasi kikubwa na kunusuru misitu yetu.

Ajenda hii ya uchumi wa kijani ni moja ya mambo tunayoweza kutumia katika kubadilisha hali ya maisha ya wananchi. Nafahamu ili kuifanikisha agenda hii kutakuwepo vizingiti vingi. Natambua namna tulivyojipanga na namna mlivyo na ari ya kuona tunafanikiwa.
 
Jitumeni kwa bidii katika kuhakikisha mkakati huu unafanikiwa na pia sisi kwa upande wetu tupo nanyi kuhakikisha kazi hii kubwa iliyopo mbele yenu inafanikiwa. Aidha, nchi yetu inahitaji watu wenye nia kama ninyi na kwa hakika hakuna wananchi wasiopenda kuona taifa letu linabakia na rasilimali zake kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Kabla ya sijahitimisha, napenda kwa mara nyingine niwashukuru kwa dhati Taasisi ya Uongozi kwa kubuni wazo zuri la Jukwaa la Uchumi wa Kijani. Mmefanya kazi nzuri na sote hapa ni mashahidi wa namna mlivyojipanga kushirikisha jamii nzima katika kufanikisha mkakati huu.
 
Ni matumaini yangu kwamba Jukwaa la Uchumi wa Kijani ninalolizindua leo litatoa fursa ya kubainisha na kuchochea ushirikiano utakaoweza kuongeza kasi ya mabadiliko ya ukuaji wa uchumi wa kijani. Kupitia jukwaa hili, watunga sera, watoa maamuzi, na watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii wataweza kubainisha, kushawishi na kushughulikia changamoto muhimu katika kipindi cha kuelekea katika uchumi wa kijani.
 
Nafarijika kuwaona wadau mbalimbali hapa leo, ikiwa ni pamoja na wawakilishi kutoka serikalini, sekta binafsi, vyama vya kiraia, na washirika wa maendeleo.  Jukwaa la Uchumi wa Kijani lazima liwe na uwezo wa kutoa fursa kwa makundi haya kujadili na kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijani nchini Tanzania.
 
Kwa maneno haya machache, sasa natamka kwamba Jukwaa la Uchumi wa Kijani limezinduliwa rasmi.
 
Asanteni kwa kunisikiliza
 

Array
 

<< Back to Announcements Archive.