BALOZI SOKOINE ATEMBELEA KIWANDA CHA KUREJEREZA TAKA ZA ELEKRONIKI

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Sokoine, ametembelea kiwanda cha urejerezaji (recycling) kinachojengwa Kisarawe mkoani Pwani ambapo amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kufanya biashara na kusaidia katika kutunza mazingira.

Sokoine ameyasema hayo jana mbele ya uongozi wa kampuni ya Chilambo General Trade Company inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Gideon Chilambo alipojionea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo ambayo hukusanya vifaa mbalimbali vilivyotumika na kuviuza hapa nchini na nchi za nje kwa ajili ya kufanyiwa urejereshaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Chilambo alitaja vifaa mbalimbali ambavyo hukusanywa na kampuni yake vikiwemo chuma chakavu, betri mbalimbali zilizotumika, vifaa mbalimbali vya mawasiliano, vifaa vya kompyuta, vya kuchapishia (printers), mashine  za kurudufia (photo-copiers), na vinginevyo hususani vile ambavyo vinatokana na plastiki na vyuma vya aina mbalimbali kama vile shaba na kadhalika.

Mkurugezi huyo aliongeza kwamba kampuni yake hiyo iliyosajiliwa mwaka 1990 ilianza kujishughulisha na huduma za maofisini pamoja na vifaa vyake (stationeries) lakini baadaye, miaka minane iliyopita, ilibadili mwelekeo wake na kuamua kujikita katika ukusanyaji wa vifaa husasani vya kieletroniki vilivyotumika.

“Kampuni yetu ambayo inapata vibali kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea na shughuli zake kwa kuzingatia taratibu zote za nchi na tumekuwa na mafanikio makubwa tangu tulivyoanza shughuli hiyo,” alisema Chilambo na kuongeza kwamba mnamo mwaka wa kwanza wa shughuli hiyo walikusaya tani zipatazo tani tano na mwaka uliofuata walikusanya tani zipatazo 55.

“Miaka inavyozidi kwenda tunakusanya tani nyingi zaidi.  Mwaka jana tumekusanya tani 18,500 na mwaka huu tunategemea kukusanya tani 100,000,” alisisitiza Chilambo huku akisema wataendelea kufuata taratibu zote za kisheria na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli katika kuendeleza viwanda na kutunza mazingira.

Hivi sasa shughuli hiyo inakusanya vitu hivyo katika ghala lililoko Pugu jijini Dar es Salaam ambalo ni dogo na makazi ya watu yanazidi kukaribia eneo hilo, hivyo kampuni imeanza mchakato wa kujenga kituo kama hicho huko Kisarawe.

Katika kupunguza changamoto za biashara hiyo, Chilambo alisema kampuni yake hivi sasa inawasiliana na makampuni ya nchi za nje ili kupata uwezekano wa makampuni hayo kuja kuwekeza nchini na kufanya miradi ya urejereshaji hapa badala ya kukusanya vitu husika na kuvisafirisha nje.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Sokoine, alipongeza shughuli yote  ya kampuni hiyo kwa kufuata tararibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ya serikali na kuchangia katika kutunza mazingira kwa kukusanya malighafi hizo ambazo zingeweza kugeuka na kuwa takatakana hivyo kuathiri mazingira nchini.

“Serikali iko pamoja na wajasiriamali wote nchini ambao wanajituma katika kutafuta mazingira bora ya shughuli zao ikiwa ni pamoja na kutafuta utaalam nchi za nje na kuja kuwaelimisha wananchi wengine juu ya kile wanachokifanya,” alisema Sokoine.