CHANGAMOTO YA KUPUNGA KWA MAJI MTO MARA KUPATIWA UFUMBUZI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amewakumbusha watendaji wa Wilaya ya Serengeti wajibu wao wa kipekee wa ulinzi katika hifadhi ya mbuga ya Serengeti kwakuwa Wilaya yao imebeba jina linalojulikana duniani kote ikiwa ni pamoja na eneo maalumu la wanyama aina ya Nyumbu ambao huvuka kwenda upande wa pili na kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii.

Waziri Makamba ameyasema hayo leo Wilayani Serengeti mara baada ya kufanya ziara ya kikazi Wilayani hapo kujionea uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira na kutembelea eneo la mto Mara eneo ambalo ni muhimu sana ki-ikolojia.

Katika kikao na viongozi wa Wilaya hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Bw. Wiliam Mwakilema aliainisha kuwa mtiririko wa maji katika Mto Mara kutoka chanzo chake kikuu katika Milima ya Mau nchini Kenya kimepungua kutokana na shughuli za kibinadamu na matumizi mengine yasiyoendelevu jambo linalohatarisha kupungua kwa mtiririko wa maji katika Mto Mara kwa kipindi kirefu, eneo ambalo ni kivutio pekee cha wanyama wanaohama dunia.

Katika kutatua tatizo hilo Waziri Makamba amesema kuwa masuala ya mazingira ni mtambuka hivyo Ofisi yake yenye dhamana na kusimamia hifadhi ya Mazingira nchini itafanya ziara ya kikazi nchini Kenya kwa lengo la kujadiliana na kupata ufumbuzi wa haraka juu ya jambo hilo.

“Sisi na wenzetu wa Kenya tumeingia mkataba mwaka 2013 wa matumizi sahihi ya rasilimali katika Mto Mara na kutunza ikolojia yake, kwa kushirikiana na Mawaziri wenzangu wa Maji na Maliasili na Utalii, tutafanya ziara nchini Kenya ili kwapamoja tupate ufumbuzi wa jambo hili ikiwa ni pamoja na Ziwa Chala, Ziwa Jipe na Ziwa Natroni ambayo yote yako pande mbili yaani Tanzania na Kenya.”

Waziri Makamba amesema Serikali itahakikisha maslahi ya Nchi yanalindwa kwa njia za ki-diplomasia na kuhakikisha Mto Mara unatiririsha maji kipindi chote cha mwaka.

Waziri Makamba amehitisha ziara yake Mkoani Mara na amewasili Mkoani Arusha ambapo atakuwa na vikao wa wadau wa hoteli mbalimbali na kambi za uwindaji kwa lengo la kuweka mikakati ya kuhifadhi mazingira maeneo ya mbugani.