Article 2

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Gulamhafeez Mukadamu, Mwenyekiti wa ALAT na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga

Mheshimiwa Stephen Peter Mhapa, Makamu Mwenyekiti wa ALAT na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mheshimiwa Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI;Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;Waheshimiwa Wabunge mliopo hapa;

 

Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na

Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya;

 

Waheshimiwa Madiwani wa Dar es Salaam, mkiongozwa

na Mstaiki Meya Isaya Mwita;

 

Mstahiki Meya wa Zanzibar pamoja na Viongozi mbalimbali

kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;

Mhandisi Mussa Iyombe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI;

Prof. Faustin Kamuzora, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais;

Bwana Abdallah Ngodu, Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT;

Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya;

Wawakilishi wa Jumuiya za Serikali za Mitaa kutoka

Nchi za Afrika Mashariki mliopo;

 

Wawakilishi wa Wadhamini kutoka Makampuni

na Mashirika ya Serikali na Yasiyo ya Kiserikali,

 

Wawakilishi wa Vikundi vya Wajasiriamali;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, ambaye ametupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, nakushukuru sana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (Association of Local Government Authorities of Tanzania – ALAT), Mheshimiwa Mukadamu, kwa kunialika kufungua Mkutano huu Mkuu wa 33 wa ALAT. Nasema Ahsante sana.

 

Natambua baadhi yenu hapa mmesafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano huu, ambao awali ulipangwa kufanyika Jijini Mbeya, lakini siku za mwishoni ukalazimika kuhamishiwa hapa Dar es Salaam. Hivyo basi, kwanza, napenda kuwapa pole kwa uchovu wa safari. Lakini pili, kama mnavyofamu, mimi pamoja na kuwa na majukumu ya Urais, nina dhamana kwenye Wizara ya TAMISEMI; hivyo basi, napenda niwakaribishe wajumbe wote hapa Dar es Salaam na katika Mkutano huu wa 33 wa ALAT. Karibuni sana ndugu wajumbe.

 

Napenda pia hapa mwanzoni kabisa nimshukuru Mwenyekiti wa ALAT Taifa kwa salamu za pongezi alizozitoa kwangu, hususan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Namshukuru pia kwa pongezi zake kuhusu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Nasema ahsante sana. Mmezidi kutupa moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii. Lakini nami ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza, wewe Mheshimiwa Mwenyekiti na Makamu wako, Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri zote nchini kwa kuchaguliwa kwenu. Napenda niwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana nanyi kwa karibu katika kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi na nchi yetu kwa ujumla.