HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20

 1. UTANGULIZI

         Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako Tukufu kupokea taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2018/19; na Malengo ya Ofisi ya mwaka 2019/20, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2019/20.

 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kuwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa mwaka 2019/20 mbele ya Bunge lako Tukufu. Aidha, ninamshukuru kwa dhati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kusimamia masuala ya Muungano na Mazingira. Pia, ninapenda kutoa pongezi kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wake makini na thabiti. Mafanikio hayo yanajidhihirisha katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ya maendeleo. Mafanikio hayo ni dalili tosha kuwa nchi ipo katika njia sahihi ya kufikia malengo tuliyojiwekea katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ya kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa dhati ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo anayotupa katika kusimamia masuala ya Muungano na kuhifadhi Mazingira. Uongozi wake thabiti unadhihirishwa na matokeo ya kazi nzuri inayofanywa ya kuudumisha Muungano wetu pamoja na kuhifadhi na kusimamia Mazingira. Aidha, kwa namna ya pekee ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri anayofanya ya kuuenzi na kuudumisha Muungano wetu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninamshukuru na kumpongeza Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa kisera katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kipindi cha mwaka 2019/20. Aidha, nampongeza kwa uongozi wake thabiti katika kusimamia shughuli za Serikali ndani na nje ya Bunge lako Tukufu. Pia ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote kwa ushirikiano walionipa katika kutekeleza majukumu ya kusimamia shughuli za Muungano na Mazingira.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa shukrani na pongezi za dhati kwa Bunge lako tukufu kwa kazi nzuri ambayo limeifanya kwa kipindi cha uongozi wako. Aidha, ninakupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuliongoza Bunge letu kwa hekima na busara kubwa. Ninampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.), Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kukusaidia kuliongoza Bunge letu kwa weledi na uadilifu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mheshimiwa Suleiman Ahmed Saddiq (Mb.) na Makamu wake Mhe.Kanali (Mst.) Masoud Ali Khamis (Mb.) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.) na Makamu Mwenyekiti Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb.) pamoja na Waheshimiwa wajumbe wa Kamati hizo kwa kupokea, kujadili na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2019/20.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa ndugu, marafiki na wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini, kwa kifo cha Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani aliyekuwa Mbunge wao kilichotokea mwezi Julai, 2018 na Mheshimiwa Kasuku Bilago aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu kilichotokea mwezi Mei, 2018. Aidha, ninatoa pole za dhati kwa wananchi kwa ujumla kwa kuwapoteza ndugu zao na mali kutokana na ajali na maafa yaliyotokea sehemu mbalimbali hapa nchini. Ninaomba Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninawapongeza wabunge wote waliochaguliwa na kuteuliwa kisha kuapishwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha. Uadilifu wao na tabia ya kujituma na kufanya kazi kwa bidii ndio sababu kubwa ya kuwa sehemu ya wawakilishi wa wananchi katika Bunge hili tukufu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba kutoa maelezo ya utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha mwaka 2018/19 na malengo ya mwaka 2019/20.

 

 1. UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2018/19

Makusanyo ya Mapato kwa Mwaka 2018/19

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais haina vyanzo vya mapato. Hata hivyo, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira hadi kufikia Machi, 2019 lilikuwa limekusaya mapato ya jumla ya sh. 10,430,060,727.00 kutokana na tozo na faini.

 

Bajeti Iliyoidhinishwa kwa Mwaka 2018/19

 

Fungu 26

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, jumla ya Sh. 6,485,991,000.00 ziliidhinishwa kwa ajili ya Fungu 26. Kati ya fedha hizo, Sh. 5,432,325,578.05 zilikuwa ni ajili ya Matumizi Mengineyo na Sh. 1,053,666,000.00 zilikuwa za Mishahara.

 

Fungu 31

 1. Kwa upande wa Fungu 31 Sh.15,065,422,523.28 Kati ya fedha hizo Sh. 10,002,082,523.28 ni za Matumizi ya Kawaida na Sh. 5,063,340,000.00 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Fedha za Matumizi Mengineyo zinajumuisha Sh. 3,017,072,000.00 ruzuku ya mishahara kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

 

Fedha Zilizopokelewa na Kutumika Hadi Machi, 2019

 

Fungu 26

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2019, jumla ya Sh. 4,572,810,578.05 zilipokelewa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yaliyopo chini ya Fungu 26. Kati ya fedha hizo Sh. 3,911,669,578.05 zilipokelewa kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Sh. 661,141,000.00 kwa ajili ya Mishahara. Aidha, hadi Machi, 2019, jumla ya Sh 4,365,447,196.20 zilikuwa zimetumika. Kati ya fedha hizo kiasi Sh. 3,704,306,196.20 zilitumika kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Sh. 661,141,000.00 kwa ajili ya Mishahara.

 

Fungu 31

 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2019 Fungu 31 lilipokea jumla ya Sh. 7,937,894,492.78 ambayo ni sawa na asilimia 52.7 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo Sh. 5,405,152,561.18 zilipokelewa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. 2,400,099,489.50 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha zilizopokelewa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, kiasi cha Sh. 1,652,371,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara, Sh. 2,331,102,003.28 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Sh. 1,554,322,000.00 ni fedha za ruzuku kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC. Aidha, Ofisi imetumia jumla ya Sh. 7,266,452,050.68 sawa na asilimia 91.5 ya fedha zilizopokelewa. Kiasi hiki kinajumuisha fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida Sh. 5,405,152,561.18. na Fedha za Miradi ya Maendeleo Sh.1,861,299,489.5. Fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida zilizotumika zinajumuisha, Sh. 1,554,322,000.00 ruzuku ya Mishahara kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi – CCM (2015 – 2020); Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals – SDG 2030); Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997; Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004; na Maelekezo na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Viongozi Wakuu wa nchi.

 

MASUALA YA MUUNGANO

 

 1. Mheshimiwa Spika, Muungano wetu ndio utambulisho wa Taifa letu na kielelezo cha umoja wetu. Bila Muungano hakuna Tanzania. Ili Kuuenzi na kuuimarisha Muungano Ofisi imeendelea kutekeleza majukumu ambayo imekabidhiwa kikatiba na kisheria ya kuratibu utekelezaji wa masuala ya Muungano na kuimarisha ushirikiano katika masuala yasiyo ya Muungano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Katika mwaka 2018/19, kazi zifuatazo zilitekelezwa: – Kuratibu vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano; Kuratibu utekelezaji wa masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa; Kuratibu masuala yasiyo ya Muungano ili kuimarisha ushirikiano kati ya SMT na SMZ; na Kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano.

 

Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi iliratibu na kufanya kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano tarehe 9 Februari, 2019 Jijini Dodoma. Kikao hiki kilitanguliwa na vikao vya Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ tarehe 6 Februari, 2019; Makatibu Wakuu wa SMT na SMZ tarehe 8 Februari, 2019; na Mawaziri wa SMT na SMZ tarehe 9 Februari, 2019.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hoja zilizojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na: – Mapendekezo ya Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano; Mwongozo wa Ushirikishwaji wa SMZ kwenye Masuala ya Kimataifa na Kikanda; na Hoja za Fedha na Biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Kikao hicho kilikuwa na mafanikio yafuatayo: – Kupitishwa kwa Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano wenye lengo la kuimarisha na kuongeza ufanisi wa vikao vya Kamati ya Pamoja ikiwa ni pamoja na kufuatilia maagizo na maelekezo yanayotolewa na Kamati hiyo. Utaratibu huo pia, umeainisha Kamati mbili ambazo ni Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala zilizopewa jukumu la kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazohitaji utatuzi wa haraka badala ya kusubiri utaratibu wa kawaida wa vikao vya Kamati ya Pamoja vya SMT na SMZ. Kamati hizo zitawasilisha taarifa za utekelezaji katika vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika Kikao hicho pia ulipitishwa Mwongozo Kuhusu Ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda. Mwongozo huo umezingatia maeneo ya mikutano ya kimataifa na kikanda, nafasi za masomo ya elimu ya juu na mafunzo mengine nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada na mikopo ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
 2. Mheshimiwa Spika, changamoto ya ongezeko la Gharama za Umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO ilipatiwa ufumbuzi ambapo imekubalika kuwa, kodi ya ongezeko la thamani (Value Added Tax-VAT) itatozwa kwa kiwango cha asilimia sifuri (0%) kwenye umeme unaouzwa na TANESCO. Vilevile, malimbikizo ya deni la VAT lililokuwa limefikia Sh. Bilioni 9 kwa shirika la ZECO kwenye umeme uliouzwa na TANESCO limefutwa.
 3. Mheshimiwa Spika, kikao cha Kamati ya Pamoja pia kilijadili na kuzipatia ufumbuzi hoja za biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ambazo ni: – Gharama za kushusha mizigo (landing fees); Viwanda vya Zanzibar kupata leseni kutoka Wakala wa Usajili na Utoaji Leseni za Biashara (Business Registrations Licensing Agency-BRELA); na Upatikanaji wa fursa za ushiriki katika miradi ya maendeleo ya viwango na ubora wa bidhaa na maendeleo ya wajasiriamali.

 

Uratibu wa Masuala ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa

 1.  Gawio kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kupata gawio la asilimia 4.5 ya fedha za Misaada ya Kibajeti (Government Budget Support – GBS); faida ya Benki Kuu; Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo; na kodi ya mapato yatokanayo na ajira (Pay As You Earn – PAYE). Hadi kufikia Machi, 2019 jumla ya Sh. bilioni 79 zimepelekwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 14.00 ni PAYE, Sh. bilioni 1.4 ni fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Sh. bilioni 5.64 ni fedha za Misaada ya Kibajeti (GBS) na Sh. bilioni 15.75 ni gawio la Benki Kuu.

 

 1.  Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Zanzibar
 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Ofisi imefanya ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo 16 kati ya 32 yaliyopo Unguja, Zanzibar. Majimbo hayo ni Nungwi, Mkwajuni, Chaani, Donge, Mahonda, Bumbwini, Mfenesini, Bububu, Welezo, Mwera, Fuoni, Kijitoupele, Mwanakwerekwe, Kiembesamaki, Paje na Makunduchi. Matokeo ya ufuatiliaji huo yanaonesha kuwa, miradi mingi ikiwemo ya maji na umeme inakidhi mahitaji kwa kuongeza huduma muhimu za kijamii na hivyo kuboresha maisha ya wananchi.

 

 1. Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
 1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwawezesha wananchi wa pande zote mbili za Muungano kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo. Miradi na Programu hizo zimefanikiwa kuinua hali ya wananchi, kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato na kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii wa pande zote mbili za Muungano. Miradi hiyo hufadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo. Katika mwaka 2018/19 utekelezaji wa Miradi na Programu hizo ni kama ifuatavyo: –

 

 1. Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tanzania Social Action Fund – TASAF);
 2. Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (Market Infrastructure, Value Addition and Rural Finance – MIVARF);
 3. Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA);
 4. Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula (Land Degradation and Food Security- LDFS); na
 5. Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (Expanded Rice Production Project – ERPP).

 

 

Uratibu wa Masuala Yasiyo ya Muungano Kati ya SMT na SMZ

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar imeendelea kuhamasisha Sekta zisizo za Muungano za SMT na SMZ kukutana na kujadili masuala yanayohusu Sekta zao, kubadilishana utaalam na wataalam ili kuleta ufanisi na uwiano wa maendeleo kwa pande mbili za Muungano. Katika kipindi hiki vikao tisa (9) vimefanyika.

 

Elimu ya Muungano kwa Umma

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi imeendelea kuelimisha Umma kuhusu umuhimu na faida zinazotokana na Muungano kupitia vyombo vya habari ikiwemo redio, televisheni na magazeti.

 

HIFADHI ENDELEVU YA MAZINGIRA

 

 1. Mheshimiwa Spika, Sekta zote za uzalishaji mali zinategemea mazingira na hivyo kufanya sekta hii kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Hata hivyo shughuli zisizo endelevu zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na kusababisha; Uharibifu wa ardhi; Ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini; Uchafuzi wa mazingira; Upotevu wa bioanuai na makazi; Uharibifu wa mifumo ikolojia ya majini; Uharibifu wa misitu; Mabadiliko ya tabianchi; Kuongezeka kwa Viumbe Vamizi; Kuongezeka kwa Taka za Kielektroniki; Kuongezeka kwa taka za kemikali; Kuwepo kwa uchafuzi utokanao na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi; na Kukosekana udhibiti wa mazao yatokanayo na Teknolojia ya uhandisi jeni.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya nchi yetu na kukabiliana na changamoto za mazingira nchini, Ofisi imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria na Mikakati mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na mikataba ya kimataifa ya mazingira pamoja na utoaji wa elimu kuhusu mazingira. Katika kutekeleza azma hiyo kwa mwaka 2018/19 yafuatayo yamefanyika; –

 

Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na Mkakati wa Utekelezaji

 1. Mheshimiwa Spika, mwaka jana niliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Ofisi inaendelea na hatua za kuboresha Sera ya Mazingira ya Taifa ya Mwaka 1997 na Mkakati wa utekelezaji. Aidha, katika mwaka 2018/19 rasimu ilijadiliwa katika ngazi ya Sekretariati ya Baraza la Mawaziri. Kwa kuwa Sera hii ni mtambuka pamoja na maoni mengine ushauri uliotolewa na Sekretarieti ilikubaliwa kupata maoni zaidi kutoka kwa wadau. Kazi hiyo imefanyika na baada ya kujiridhisha kuwa maoni ya wadau yamezingatiwa Rasimu ya Sera itajadiliwa katika ngazi inayofuata ambayo ni kikao cha Makatibu Wakuu (Inter – Ministerial Technical Committee – IMTC).

 

Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi inaratibu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ambayo ilitungwa mwaka 2004. Katika kipindi cha utekelezaji wa Sheria hii changamoto kadhaa zimejitokeza ikiwemo kutoandaliwa kwa baadhi ya Kanuni na Miongozo; uwezo mdogo wa Taasisi zinazosimamia utekelezaji wa Sheria ikiwemo Wizara za Kisekta na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na uelewa mdogo kuhusu wajibu na majukumu ya wadau katika utekelezaji wa Sheria hii. Ili kukabiliana na changamoto zipo juhudi mbalimbali ambazo ofisi imepanga kuchukua ikiwa ni pamoja na kutekeleza Mradi wa Kujenga Uwezo wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden. Mradi huu una thamani ya Dola za Marekani Milioni tatu (3) na utatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu (2019/20 -2021/22). Baadhi ya shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuandaa Kanuni na Miongozo; kuendesha mafunzo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wizara za Kisekta; na kuanzisha mfumo wa utoaji vyeti na leseni za mazingira kwa njia ya mtandao. Hadi kufikia sasa, Ofisi imeratibu uteuzi wa Wakaguzi wa Mazingira wapatao 487 watakaosaidia kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya usimamizi wa mazingira katika ngazi ya Serikali za Mitaa.

 

Tuzo ya Rais ya Hifadhi ya Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi imekamilisha Mwongozo wa kushiriki Tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Mazingira. Awali Tuzo hii ilihusu masuala ya kupanda na kutunza miti na kuhifadhi vyanzo vya maji pekee. Maboresho ya tuzo yamefanyika ili kuwa na mtazamo mpana wa hifadhi ya mazingira. Maboresho hayo yameongeza masuala yafuatayo: – Uzalishaji endelevu viwandani, matumizi ya nishati mbadala, uchimbaji madini endelevu, kilimo na ufugaji endelevu, usimamizi wa taka, afya na usafi wa mazingira.

 

Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Ofisi imekamilisha rasimu ya Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini na sasa kinachofanyika ni kupitisha rasimu hiyo katika ngazi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Kamati ya Mazingira ya Baraza la Mawaziri kabla ya kuwasilishwa Bungeni ili kukidhi matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu 175 (1).

 

Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2018/19, Ofisi iliainisha mapendekezo ya maeneo ya kufanyiwa marekebisho katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, 2004 ili kuwezesha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira kufanya kazi kwa ufanisi. Kwa kuwa Sera ya Taifa ya Mazingira (1997) inafanyiwa maboresho, kipaumbele ni kukamilisha Sera ili maeneo yote yatakayohitaji maboresho kwenye Sheria yafanyike kwa pamoja. Ni matarajio yetu kuwa Maboresho ya Sera pamoja na Sheria yatasaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali kusimamia masuala ya mazingira nchini na hivyo kuwa na maendeleo endelevu.

 

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani

 1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kimataifa yatafanyika nchini China katika mji wa Hangzhou kaulimbiu ikiwa ni Uchafuzi wa Hewa (Air Pollution). Kitaifa maadhimisho haya yatafanyika Mkoani Mwanza. Uteuzi wa Mkoa wa Mwanza umezingatia changamoto zinazolikabili jiji hili ikiwa ni pamoja na uwepo wa uharibifu wa ardhi katika Bonde la Ziwa Victoria pamoja na uharibifu wa mazingira ya ndani ya Ziwa hilo unaosababishwa na shughuli za kijamii na kiuchumi. Kufanyika kwa maadhimisho ya kitaifa Mkoani humo kutatoa fursa kwa wananchi wa Mkoa huo na Mikoa jirani kuelimishwa na kuhamasishwa kuhifadhi mazingira ya Bonde la Ziwa Victoria pamoja na mazingira yake.

 

Kupunguza Matumizi ya Mkaa Unaotokana na Miti

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na jitihada za kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali kuandaa mipango kazi kwa kila Taasisi ya kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti. Aidha, Ofisi imeendelea kushirikiana na wadau wa mazingira kutoa mafunzo kwa washindi wa Tuzo ya Teknolojia ya Mkaa Mbadala kwa lengo la kukuza teknolojia na ubunifu wao ili bidhaa zao ziweze kuwa za kiwango kinachokubalika kitaalam na kibiashara na hatimaye kuwafikia wananchi wengi.

 

Matumizi ya Mifuko ya Plastiki

 1. Mheshimiwa Spika, ili kutimiza azma ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki Ofisi ilihamasisha wajasiriamali na wawekezaji kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala ikiwemo vikapu vya asili, mifuko ya karatasi na nguo ili kutumia fursa hiyo kukidhi mahitaji ya soko. Kampeni za uhamasishaji zilifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza kwa lengo la kuwatambua wadau wanaozalisha mifuko mbadala na kupata maoni kuhusu namna ya kujenga mazingira wezeshi kwa wadau kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mifuko mbadala.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kufuatia tamko la Serikali la kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, uuzaji, usambazaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki kuanzia tarehe 01 Juni, 2019, Ofisi imeandaa kanuni zitakazochapishwa katika Gazeti la Serikali chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kutoa adhabu kwa kila mtu atakayekiuka matakwa ya Kanuni. Vilevile, Ofisi imeunda Kikosi Kazi cha Taifa kwa ajili ya kusimamia uzingatiaji wa Kanuni. Kikosi kazi hicho kinahusisha wajumbe kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege, Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kikao na wawekezaji wa mifuko mbadala kilichofanyika tarehe 15 Aprili, 2019 wamenihakikishia kuwa wana uwezo wa kuzalisha mifuko mbadala kukidhi mahitaji ya nchi. Aidha, Ofisi itaendelea kuhamasisha umma juu ya jambo hili ili liweze kuzingatiwa. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono jitihada hizi kwa mustakabali wa nchi yetu.

 

Mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi (Invasive Species)

 1. Mheshimiwa Spika, Viumbe Vamizi ni changamoto kubwa na mpya ya mazingira nchini. Viumbe hawa husababisha athari kubwa katika uchumi hususan katika sekta kuu za uzalishaji kama vile, kilimo, uvuvi, mifugo, maji, maliasili na utalii na hivyo kuathiri ajira na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Pia huathiri afya ya binadamu, mifugo pamoja na mazingira kwa kuharibu mifumo ikolojia. Tafiti zinaonesha kuna takriban aina 220 ya Viumbe Vamizi nchini na Tanzania imeathirika zaidi ya nchi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kwa kuzingatia hali hiyo hatua za haraka zisipochukuliwa kuwadhibiti, uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi utaendelea kuathirika kwa kasi kubwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ili kukabiliana na athari hizo katika mwaka 2018/19, Ofisi iliunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi. Mkakati huo utasaidia kudhibiti kuongezeka na kusambaa kwa viumbe hawa nchini ambao ni tishio kubwa kwa bioanuai. Mpango Mkakati huo umebainisha hatua za kuchukua ili kukabiliana na changamoto hii pamoja na kuainisha majukumu ya kila Sekta husika. Mkakati huu utajadiliwa katika kikao cha Kamati ya Mazingira ya Baraza la Mawaziri ili kuwa na uelewa wa pamoja wa majukumu ya Serikali na wadau katika utekelezaji wa mkakati huo.

 

 

Usimamizi wa Taka Zenye Madhara

 1. Mheshimiwa Spika, taka hatarishi zinazalishwa viwandani, migodini, hospitalini na baadhi ya maeneo ya biashara. Ofisi imeendelea kudhibiti uzalishaji na utupaji wa taka zenye madhara kwa mujibu wa Kanuni za Udhibiti wa Taka zenye Madhara za mwaka 2009. Aidha, Serikali inapitia utaratibu wa kusimamia taka zenye madhara kwa lengo la kuziboresha ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kudhibiti usafirishaji wa vyuma chakavu nje ya nchi. Vile vile, Serikali imeimarisha udhibiti katika vituo vya forodha pamoja na kuimarisha ushirikiano na Taasisi zenye dhamana. Lengo ni kupunguza na kuondoa biashara holela ya vyuma chakavu inayochangia kuhujumu na kuharibu miundombinu. Aidha, kwa kushirikiana na maafisa mazingira wa Halmashauri na Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeendelea kutoa vibali vya kukusanya, kuhifadhi, kusafirisha na kurejeleza taka kwa kampuni zilizokidhi vigezo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 vibali 87 kati ya maombi 107 vimetolewa.

 

Elimu kwa Umma Kuhusu Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi ilikamilisha maandalizi ya Mfumo wa Taarifa kuhusu Mazingira (Central Environmental Information System) utakaoendana na mfumo wa teknolojia ya simu kuwawezesha watumiaji kupokea na kutoa taarifa zinazohusu masuala ya Mazingira.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na: Maandalizi ya Kutangaza Maeneo ya Mazingira – Lindwa na Nyeti ikiwa ni pamoja na kuandaa orodha, kuunda Kamati ya Kitaifa, Kuandaaa vigezo na kujadili maeneo yanayopendekezwa; Kuendelea na juhudi za Kuokoa Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu; Kuandaa mapendekezo ya kukabiliana na changamoto zinazokabili utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji miti kwa kushirikiana na Sekta husika; Tathmini ya Mazingira Kimkakati (TMK); Uratibu na Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa na ya Kikanda ya Mazingira; Udhibiti wa Taka Ngumu Nchini hususan kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji katika Taka Ngumu ili kuhamasisha uwekezaji na kuongeza jitihada za kuboresha usimamizi wa taka hapa nchini. Katika utekelezaji wa Mwongozo huo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ina jukumu la muhimu sana kufuatilia utekelezaji wa Mwongozo huo ili kuleta ufanisi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia katika mwaka 2018/19 Ofisi imeratibu shughuli za Mfuko wa Mazingira wa Dunia (Global Environmental Facility) kwa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mitatu iliyopata ufadhili kutoka Mfuko huo na kuandaa miradi mitano (5) na kuiwasilisha katika Sekretarieti ya GEF kwa ajili ya kupata ufadhili chini ya Awamu ya Saba ya Mfuko (GEF – 7th Replenishement Cycle) ambapo katika awamu hii Tanzania imetengewa fedha kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 24.

 

BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

 1. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ambalo ndio msimamizi mkuu wa uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 limeendelea kutekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

 

Uzingatiaji na Usimamizi wa Sheria ya Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inazingatiwa ipasavyo katika kutekeleza shughuli za maendeleo hapa nchini, Baraza limetekeleza kazi zifuatazo:-

 

 1. Ukaguzi wa Maeneo ya Uwekezaji na Mazingira
 2. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Baraza limefanya ukaguzi katika viwanda, machinjio ya wanyama, migodi (yakiwemo machimbo ya mchanga na kokoto), hifadhi ya vyanzo vya maji, mashamba, vituo vya mafuta, maghala ya kuhifadhi kemikali na taka hatarishi, madampo, hoteli, mifumo ya maji taka, taasisi za elimu na afya, majengo ya biashara na makazi ili kupima uzingatiaji na usimamizi wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini. Katika ukaguzi huo jumla ya miradi 4,853 ilikaguliwa ambapo miradi 1,627 ni ya viwanda sawa na asilimia 34. Ukaguzi huo ulibaini kuwa asilimia 40 ya miradi inazingatia Sheria na baadhi ya miradi kuwa na changamoto za kimazingira kama:- kutiririsha majitaka kwenye vyanzo vya maji na mazingira; Kutumia rasilimali za misitu ya asili kwa ajili ya kuni na majengo; Kutokuwa na mifumo ya kuhifadhi na kusimamia taka ngumu; Uzalishaji wa hewa chafu; Udhibiti na Uhifadhi duni wa taka hatarishi; Upigaji wa kelele na mitetemo zaidi ya viwango vinavyokubalika kimazingira; na baadhi ya viwanda kuanzishwa kwenye makazi ya watu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Baraza limechukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191, kwa miradi iliyokiuka Sheria na Kanuni zake. Hatua hizo ni pamoja na kutoa ushauri, maelekezo, maonyo, amri za katazo, amri za urejeshaji wa mazingira na kuwafikisha mahakamani.

 

 1. Kushughulikia Malalamiko ya Kimazingira
 2. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Baraza limeendelea kupokea malalamiko yanayohusu uchafuzi wa mazingira kutoka kwa wananchi na kuyashughulikia kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 na Kanuni zake. Katika kipindi hiki zaidi ya malalamiko 701 yamepokelewa kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuyapatia ufumbuzi. Baadhi ya malalamiko yalihusu:- Kelele kutoka katika karakana; Nyumba za ibada; Kumbi za starehe; Viwanda na utengenezaji wa matofali; Utiririshaji wa majitaka kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya uzalishaji; Uchimbaji wa mchanga katika vyanzo vya maji na maeneo mengineyo; na uchafuzi wa mazingira kutokana na uanzishwaji wa machinjio ya wanyama kwenye makazi ya watu.

 

Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM)

 1. Usajili wa Miradi na Utoaji wa Vyeti vya Mazingira
 2. Mheshimiwa Spika, ili kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika utoaji wa vyeti vya Tathimini ya Athari kwa Mazingira katika Miradi ya Maendeleo utaratibu wa utoaji wa vyeti hivyo umeboreshwa. Baraza limeweka utaratibu wa kutoa Kibali cha Awali cha Mazingira (Provisional Environmental Clearance) ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na maandalizi ya awali ya mradi wakati mchakato wa TAM unaendelea. Kibali hicho kinatumika kwa miradi ya viwanda, kilimo na miradi mingine ya kipaumbele kwa Serikali. Mpaka sasa jumla ya Vibali saba (7) vya Awali vya Mazingira vimetolewa. Utaratibu huu utasaidia kuharakisha uwekezaji katika Sekta ya viwanda nchini. Vilevile Serikali inaandaa utaratibu utakaowezesha kuwa na namba za simu (hot lines) zitakazowezesha wawekezaji kutoa taarifa au malalamiko kuhusiana na maombi wanayoyawasilisha ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati. Utaratibu huu utawezesha Ofisi kufanyia kazi maoni yanayotolewa na hivyo kuboresha taratibu zinazotumika kutoa vyeti hivi kila inapohitajika.

 

Katika mwaka 2018/19 Baraza limesajili jumla ya miradi 1,254 ya maendeleo kwa ajili ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na Ukaguzi wa Mazingira, ambapo jumla ya miradi 455 ilikamilika na kupatiwa vyeti vya mazingira. Vilevile, Ofisi imefanya maboresho ya Kanuni katika mchakato wa TaM na kupunguza idadi ya siku. Miradi yenye athari ndogo kwa mazingira itatumia jumla ya siku 35 tu kupata cheti ambapo siku 21 zitakuwa kwa ajili ya NEMC kukamilisha taratibu husika, na siku 14 ni kwa ajili ya Waziri mwenye dhamana ya mazingira kutoa maamuzi. Aidha, miradi yenye athari kubwa kwa mazingira itapata kibali cha muda ndani ya siku 14 na sasa mchakato wa TAM utatumia siku 88 kutoka siku 149 zilizokuwa zikitumika awali. Aidha, gharama ya usajili wa miradi ya TAM imepungua na haitozwi kwa kiwango cha asilimia ya gharama ya mradi kama ilivyokwa awali. Kwa sasa gharama za usajili wa mradi zinaanzia Sh. Milioni 4 kwa miradi midogo na kwa miradi mikubwa gharama haizidi Sh. milioni 50.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mchakato wa miradi ya kitaifa na kimataifa inakwenda kwa kasi inayokubalika, Baraza limekuwa likishauriana na wahusika katika kila hatua ya utekelezaji. Mfano wa miradi hiyo ni: Mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP). Baraza limepokea ripoti ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Kamati ya kupitia ripoti hii imeteuliwa; Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira Dodoma (Dodoma Sports Complex) ulipewa cheti cha Mazingira tarehe 31 Julai 2018; na Mradi wa kufua Umeme wa Rufiji (Rufiji Hydropower Project) umeshapatiwa cheti cha TAM. Baraza kwa kushirikiana na TANESCO litaratibu na kusimamia utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa mazingira wakati wote wa utekelezaji wa mradi.

 

 1. Kuandaa Miongozo kuhusu TAM
 2. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mchakato wa TAM unatekelezwa kwa ufanisi, Baraza kwa kushirikiana na Kituo cha Sayansi na Mazingira cha India limeandaa miongozo itakayosaidia kurahisisha mapitio ya miradi ya majengo na Sekta ya ujenzi. Miongozo hii iko katika hatua za mwisho ambapo wadau watashirikishwa kutoa maoni kabla ya kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza.

 

Aidha, Baraza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali – Mbeya, Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Chunya, Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mamlaka ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi (Mbeya) na wawakilishi wa wachimbaji wadogo kutoka Wilaya ya Chunya limeandaa utaratibu wa kurahisisha mchakato wa kuandaa maandiko ya Tathimini ya Athari kwa Mazingira kwa miradi ya wasafishaji wadogo wa dhahabu (elusion plants) katika Wilaya ya Chunya. Utaratibu huu utawapunguzia gharama za kufanya TAM wawekezaji hao wadogo katika Sekta ya madini.

 

Elimu kwa Umma Kuhusu Hifadhi ya Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Baraza limeendelea kutoa elimu kwa Umma kwa kutumia vyombo vya habari na mafunzo kwa wadau kuhusu masuala ya mazingira ili kujenga uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya mazingira. Aidha, Baraza lilishiriki katika maadhimisho mbalimbali na muhimu kimazingira ili kukuza uelewa wa jamii kwa lengo la kuboresha uwajibikaji katika kutunza na kuhifadhi Mazingira. Maadhimisho hayo ni pamoja na Siku ya Maonesho ya Viwanda na Biashara na Maonesho ya Nane Nane. Pia Baraza liliendesha warsha ya kuelimisha wadau kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni zake ambapo jumla ya wachimbaji wadogo 70 wa dhahabu pamoja na wamiliki 23 wa viwanda vya kukoboa mpunga katika Mikoa ya Mbeya na Songwe walielimishwa.

 

Ajenda ya Taifa ya Utafiti katika Mazingira (National Environmental Research Agenda – NERA)

 1. Mheshimiwa Spika, Baraza limeendelea kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Utafiti katika Mazingira (National Environmental Research Agenda – NERA) kwa kufanya tathmini ya lindimaji/dakio (catchment) la Bonde la Wami-Ruvu. Mkutano wa wadau unaandaliwa ili kutengeneza Mpango wa Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira ya dakio hilo. Vile vile, Baraza limefanya ufuatiliaji wa bomba kuu la mafuta (TAZAMA pipeline) ili kupata taarifa ya hali ya mazingira na bioanuai zilizopo na kupendekeza njia bora za uhifadhi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Baraza pia limefanya tathmini ya mmomonyoko wa fukwe za Kigamboni; utafiti wa kina kuhusiana na tatizo la kujaa kwa maji ya mvua katika makazi eneo la Mlandizi, Halmashauri ya Kibaha. Ripoti ya utafiti huo inaandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa katika Mamlaka husika kwa utekelezaji.

 

Mipango ya Hifadhi ya Mazingira Katika Maeneo Maalum

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Baraza limeendelea kuratibu shughuli zote za Hifadhi Hai (Man and Biosphere Reserves – BRs) tano (5) ambazo ni Serengeti, Ngorongoro, Ziwa Manyara, Usambara Mashariki na Jozani Chwaka Bay iliyopo Zanzibar. Aidha, Baraza limeanza maandalizi ya Kongamano la Kisayansi kuhusu Hifadhi Hai (Biosphere Reserves) Kongamano hili linatarajiwa kufanyika mwezi Agosti, 2019.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Baraza lilitembelea Mikoa sita (Singida, Tabora, Geita, Mara, Manyara na Arusha) kuthibitisha taarifa za maeneo yaliyopendekezwa kutengwa kama maeneo Nyeti na Lindwa (EPA and ESAs). Maeneo yaliyotembelewa na kuridhiwa na wananchi ili yatangazwe kuwa maeneo Nyeti ni pamoja na Msitu wa Mwalimu Nyerere na Mlima Mkendo yaliyoko Mkoa wa Mara pamoja na Singidani, Kindai na Munang yaliyoko Mkoa wa Singida. Baraza liko katika mchakato wa kuainisha na kuyapima maeneo hayo ili kupata ukubwa na ‘geographical coordinates’ kwa ajili ya kuyatambua. Aidha, mazungumzo na wadau muhimu yanaendelea ili kujiridhisha na taarifa zilizopatikana kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho ya kuyatangaza maeneo hayo kuwa maeneo Lindwa.

 

 

 1. Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni Ukaguzi wa Sampuli katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kwa lengo la kuchunguza uwepo wa viambata vya kemikali za sumu (hasa Zebaki) na utoaji wa Mafunzo kwa Wakaguzi wa Mazingira 194; Uteketezaji wa Kemikali/Taka Hatarishi.

 

Uratibu wa Miradi Inayotekelezwa kwa Fedha za Washirika wa Maendeleo Nchini

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Uratibu wa Miradi ya maendeleo katika mwaka 2018/19 Baraza limeendelea kutekeleza na kuratibu miradi miwili (2) kwa kupitia fedha za wafadhili. Miradi hiyo ni:
 2. Mradi wa Kuhifadhi Lindimaji la Bonde la Kihansi pamoja na dakio lake (Kihansi Catchment Conservation Management Project – KCCMP); na
 3. Mradi wa Kujenga Uwezo kwenye Sekta Zinazoshughulika na Nishati (Energy Sector Capacity Building Project – ESCABP).

 

MASUALA MTAMBUKA, (UTAWALA NA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU)

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Baraza imeendelea kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma sambamba na kuwawezesha watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Katika kipindi hiki watumishi wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi imefanikiwa kuajiri watumishi wapya wa kada mbalimbali kwa lengo la kujaza nafasi zilizo wazi ili kuongeza nguvukazi na kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi. Vilevile kuwawezesha wafanyakazi kushiriki katika semina, mikutano na mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo katika masuala ya mazingira. Aidha, Baraza limeboresha mifumo ya kifedha na kujiunga na Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato na Malipo Mtandao (Government e-Payment Gateway – GePG).

 

CHANGAMOTO NA MIKAKATI ILIYOPO

 1. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yetu Ofisi ilikumbana na changamoto kadha zikiwemo; – Upatikanaji wa rasilimali fedha zinazoendana na mahitaji halisi ya Ofisi; Uelewa mdogo wa wadau kuhusu masuala ya Muungano na umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira; Upatikanaji wa takwimu sahihi za mazingira; na kutokuwa na wataalam wa kutosha. Hata hivyo tulichukua hatua katika kukabiliana nazo ikiwa ni pamoja na ;- Kuandaa miradi na kuiwasilisha kwa Wadau wa Maendeleo kwa ajili ya kupata fedha za utekelezaji; Kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia redio, luninga, magazeti, machapisho, maadhimisho na maonyesho ya kitaifa kuhusu Masuala ya Muungano na umuhimu wa kuhifadhi mazingira, pamoja na kuhamasisha wadau hususan Serikali za Mitaa na sekta binafsi kushiriki katika masuala ya mazingira; Kuandaa taarifa ya Hali ya Mazingira pamoja na kuandaa maandiko ili kupata ufadhili katika eneo la ukusanyaji takwimu; kutoa mafunzo kwa wataalam pamoja na kuajiri.

 

 1. MALENGO NA MAOMBI YA FEDHA ZA MATUMIZI YA KAWAIDA NA MAENDELEO KWA MWAKA 2019/20

Masuala ya Muungano

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuuenzi Muungano katika mwaka 2019/20 Ofisi imepanga kutekeleza majukumu na malengo yafuatayo: –

 

 1. i) Kuratibu vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano pamoja na ufuatiliaji wa maelekezo na maagizo yanayotolewa katika vikao;
 2. ii) Kufuatilia utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo zinazotekelezwa pande zote za Muungano, kuhakikisha gawio la asilimia 4.5 ya fedha za Misaada ya Kibajeti (GBS), faida ya Benki Kuu, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na PAYE linapelekwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na ziara za kikazi ili kuimarisha Muungano;

iii)      Kutoa elimu ya Muungano kwa makundi tofauti ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuandaa warsha na makongamano ili kuendelea kuamsha ari ya kuuenzi, kuulinda na kuuimarisha Muungano ambao umedumu miaka 55; na

 1. iv) Kuhamasisha Wizara, Idara na Taasisi zisizo za Muungano zenye majukumu yanayoshabihiana kuendelea kufanya vikao angalau mara mbili kwa mwaka ili kupunguza changamoto za kisekta kwa ustawi wa Muungano wetu.

 

Hifadhi ya Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kuhifadhi Mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho katika mwaka 2019/20 Ofisi imepanga kutekeleza majukumu na malengo yafuatayo:-

 

Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi imepanga kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997 na Mkakati wake wa Utekelezaji. Lengo la mapitio hayo ni ni kuboresha Sera ya Taifa ya Mazingira kwa kuhakikisha masuala mapya ya kimazingira yanazingatiwa ili kujumuishwa katika Mkakati wa utekelezaji. Aidha, kwa kuzingatia maboresho ya Sera Ofisi itakamilisha Marekebisho ya Sheria ikiwa ni pamoja na kuwezesha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira kusajiliwa na kuanza kufanya kazi kama inavyostahili. Ni matarajio yetu kuwa Maboresho ya Sera pamoja na Sheria yatasaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali kusimamia masuala ya mazingira nchini na hivyo kuwa na maendeleo endelevu.

 

Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi itachapisha nakala za Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira ya Mwaka 2018 kwa lengo la kuzisambaza kwa wadau na kutoa elimu kwa umma kuhusu hali ya mazingira nchini. Vilevile Ofisi itaandaa Ripoti hiyo katika lugha nyepesi ili kurahisisha utoaji wa elimu. Ripoti hii ina takwimu na taarifa muhimu zitakazosaidia katika Mipango ya kuhifadhi mazingira nchini. Ripoti hiyo itawasilishwa Bungeni kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu 175 (1).

 

          Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Mbadala

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi itaendelea kuelimisha na kuhamasisha umma ili kuhakikisha kuwa, mkaa mbadala unatumiwa na kukubalika na watu wengi ikiwa ni pamoja na kuwa na viwango vinavyokubalika kitaaalam. Ofisi kwa kushirikiana na taasisi za elimu na za utafiti, itatumia kazi za washindi kuweka viwango vya ubora wa mkaa mbadala unaozalishwa hii ikiwa ni pamoja na: kiwango cha nishati joto (calorific values); aina ya vifungashio (packaging materials); uzito wa mkaa (density) pamoja na kujua usalama wa kiafya kwa mkaa unaozalishwa kulingana na aina ya viambata (ingredients) vinavyotumika kutengeneza mkaa husika. Pia Taasisi zote za Serikali zitahamasishwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mkaa na kuni na kuongeza matumizi ya nishati mbadala hususan gesi ya kwenye mitungi (Liquified Petroleum Gas – LPG.

 

Mifuko ya Plastiki

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi itaendelea kusimamia uzingatiaji wa Kanuni zinazoandaliwa chini ya usimamizi wa Sheria ya Mazingira, kutoa elimu na kuhamasisha wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki wa viwanda vya mifuko ya plastiki ili kuhakikisha utekelezaji wa tamko la Serikali la kupiga marufuku uingizaji, uuzaji, uzalishaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki linatekelezwa kwa ufanisi. Aidha, nichukue fursa hii kuwahimiza wawekezaji kuendelea kutumia fursa hii kuwekeza katika teknolojia ya uzalishaji wa mifuko mbadala.

 

Viumbe Vamizi

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi kwa kushirikiana na wadau itaratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi (2019 – 2029). Mkakati huo unalenga kuimarisha juhudi za Serikali kukabiliana na ueneaji wa viumbe hao na athari zake ambazo zinaendelea kuongezeka kwa kasi nchini na hivyo kuathiri sekta kuu za uchumi ambazo ndiyo msingi wa uzalishaji na ajira. Juhudi hizo zitakwenda sambamba na utoaji elimu kwa umma juu ya jambo hili ili kuhakikisha wadau wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na tatizo hili. Nachukua fursa hii kuomba wadau wa mazingira ikiwa ni pamoja na sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo, Mashirika na Asasi zisizo za Serikali kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na tatizo hili.

 

Kampeni ya Upandaji Miti

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi itaendelea kuhamasisha na kufuatilia utekelezaji wa kampeni ya upandaji miti kwa kushirikiana na Sekta zinazohusika katika Halmashauri za Wilaya Nchini ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha kufikiwa kwa malengo ya kampeni hii. Baadhi ya masuala yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kuhamasisha wananchi kupanda miti ya matunda ambayo pamoja na kuhifadhi mazingira itasaidia kukuza kipato na kuimarisha afya kwa jamii. Juhudi hizo zitakwenda sambamba na kusisitiza juu ya utunzaji wa miti ya asili.

 

 

Tuzo ya Rais ya Hifadhi ya Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali itaendesha mashindano ya Tuzo ya Rais ya Hifadhi ya Mazingira kwa kutumia Mwongozo wa Tuzo ulioboreshwa. Baadhi ya masuala yalioongezwa katika mwongozo huo ili kuuboresha ni pamoja na uzalishaji endelevu viwandani, matumizi ya nishati mbadala, uchimbaji madini endelevu, kilimo na ufugaji endelevu, usimamizi wa taka, afya na usafi wa mazingira. Aidha washindi wa Tuzo hii wanatarajiwa kupewa Tuzo zao wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, tarehe 5 Juni, 2020;

 

Uzuiaji wa Shughuli za Binadamu katika Baadhi ya Maeneo

 1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu cha 57 (1) kinakataza kutofanyika shughuli yoyote ya kibinadamu ya kudumu au ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na au utunzaji wa bahari au kingo za mito, bwawa, au miambao ya asili ya ziwa. Hata hivyo, Kifungu 57 (2) kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya mazingira kuweka miongozo ya kuendesha shughuli za binadamu ndani ya maeneo yaliyoelezwa. Kwa kuzingatia hilo Ofisi inaandaa Miongozo itakayotoa ufafanuzi kuhusu aina ya shughuli zinazoweza kutekelezwa katika maeneo hayo. Lengo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwiano kati ya uongezaji wa kipato cha wananchi pamoja na uzingatiaji wa uhifadhi wa mazingira katika eneo lililolengwa.

 

Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Maji Zinazovuka Mipaka Kati ya Kenya na Tanzania

 1. Mheshimiwa Spika, Tanzania na Kenya ni nchi jirani zinazomiliki kwa pamoja baadhi ya Maziwa na Mito ikiwemo, Ziwa Chala, Ziwa Jipe, Ziwa Natron na Mto Mara. Kwa muda mrefu nchi hizi mbili zimekuwa kwenye changamoto za matumizi yasiyo endelevu kwa rasilimali hizo na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira unaopelekea upungufu wa utiririshaji maji, kupungua kwa kina cha maji kwa baadhi ya Mito na Maziwa na kuongezeka kwa magugu maji kunakohatarisha bioanuai ya maeneo haya. Ili kukabiliana na changamoto hizo nchi za Kenya na Tanzania zimekubaliana masuala yafuatayo; Kuunda Kamati ya pamoja katika ngazi ya Wataalam na Mawaziri; Kufanya tathmini ya kina ya rasilimali za mipakani; na Kuandaa Mkataba wa usimamizi wa rasilimali hizo pamoja na Mpango wa utafutaji wa rasilimali fedha. Hadi sasa Kamati ya pamoja ya Wataalam kwa ajili ya kutoa mwongozo wa kitaalam wa usimamizi wa rasilimali za mipakani zinazomilikiwa kwa pamoja imeshaundwa na kuanza kazi.

 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Serikali itaendelea kuratibu kazi chini ya Kamati hizi kwa kushirikiana na Serikali ya Kenya.

 

Uratibu wa Usimamizi wa Mazingira Katika Ngazi ya Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa

 1. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kutekeleza Sheria ya Mazingira, Ofisi itaendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali ya Mitaa ili kuimarisha uratibu wa usimamizi wa Mazingira kwa kuhakikisha uteuzi wa wataalam wa usimamizi wa mazingira katika ngazi za Miji, Wilaya, Manispaa, Jiji na Mikoa unaendelea kufanyika. Maafisa hao ni kiungo katika utekelezaji, usimamiaji na ufuatiliaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika maeneo hayo na hivyo wana wajibu wa kushauri Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa Sheria hii. Aidha, utekelezaji, uratibu na ufuatiliaji utahusisha uundaji wa Kamati za Usimamizi wa Mazingira za Jiji, Manispaa, Wilaya, Mji, Kata, Kijiji, Mtaa na Kitongoji pamoja na kuhakikisha kuwa zinafanya kazi na uandaaji na utekelezaji wa Mipango ya Mazingira ya mamlaka ya Serikali za Mitaa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Kazi nyingine zitakazotekelezwa katika hifadhi ya mazingira ni pamoja na; –
 2. Kuendesha mafunzo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wizara za Kisekta; na kuanzisha mfumo wa utoaji vyeti na leseni za mazingira kwa njia ya mtandao;
 3. Kuratibu utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi ili kuhakikisha hali ya Mfumo Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu inaendelea kuimarika;
 4. Kuelimisha Umma kuhusu Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa (GMO) kupitia vyombo vya habari ikiwemo redio, luninga na magazeti. Vilevile, Ofisi itaandaa na kuchapisha Mkakati wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma kuhusu Hifadhi ya Mazingira;
 5. Kusimamia, Kuratibu na Kufuatilia Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ya Mazingira ambayo Tanzania ni Mwanachama na kuandaa msimamo wa nchi na kuratibu ushiriki katika mikutano ijayo ya nchi wanachama wa Mikataba ya kimataifa ya hifadhi ya mazingira;
 • Kutoa vyeti vya Tathmini ya Athari za Mazingira (TAM) kwa miradi na Tathmini ya Mazingira Kimkakati (SEA) na kufuatilia utekelezaji wa suala hili kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004;
 1. Kuratibu utekelezaji wa Mikakati iliyopo chini ya Mikataba ya Kimataifa tuliyoridhia;
 2. Kuwezesha mchakato wa kuridhia Mikataba na Itifaki za Mazingira ambazo Tanzania imesaini;
 3. Kutekeleza miradi ya hifadhi na usimamizi wa mazingira na Mabadiliko ya Tabiachi iliyopo chini ya Mikataba ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini na ufuatiliaji; na
 • Kuandaa miradi ya kuhifadhi mazingira na kuiwasilisha kwa wafadhili kwa ajili ya kupatiwa fedha kutoka kwenye Mifuko na Mashirika yanayohusika na kuhifadhi mazingira.

 

Malengo ya Baraza la Taifa la Kusimamia na Kuhifadhi Mazingira

 1. Mheshimiwa Spika, Baraza katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 limepanga pamoja na mambo mengine kutekeleza yafuatayo katika mwaka 2019/20: –
 2. i) Kufanya ukaguzi na ufuatialiaji wa Miradi ya Uwekezaji na kuchukua hatua stahiki;
 3. ii) Kuandaa na kufanya mapitio ya nyezo na miongozo mbalimbali inayohusu uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira na Kanuni zake;

iii)      Kuboresha mfumo na mchakato wa TAM ili kuwezesha upatikanaji wa vyeti kwa haraka zaidi na kuendelea  kutoa miongozo kwa wadau ili kuhakikisha TAM inazingatiwa kabla ya uwekezaji kufanyika;

 1. v) Kuendelea kusajili miradi kwa ajili ya mchakato wa TAM, kusajili wataalam wa TAM na Wakaguzi wa Mazingira pamoja na kufanya vikao vya kinidhamu;

viii)    Kufanya tathmini ya mifumo ikilojia katika bonde la maji la Rufiji katika eneo la mradi wa umeme wa Rufiji;

 • Kuendelea kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Utafiti katika Mazingira;
 1. Kufanya mapitio ya miradi inayowasilishwa na wadau ili iweze kupata ufadhili;
 2. x) Kuandaa miongozo ya usimamizi wa mazingira katika maeneo lindwa na nyeti;
 3. xi) Kufanya ufuatiliaji wa karibu wa shughuli zinazofanyika katika Mradi wa Uzalishaji Umeme wa Rufiji;

xii)     Kuimarisha Usimamizi wa taka ngumu;

xiii)    Kuongeza wigo wa mapato;

xiv)    Kuendelea na kampeni za elimu ya mazingira kwa umma.

 

Miradi ya Maendeleo

 • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 miradi mikubwa ifuatayo ya hifadhi na usimamizi wa mazingira imepangwa kutekelezwa ni: Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula Katika Maeneo Kame Tanzania; Mradi wa Kuhimili Athari ya Mabadiliko ya Tabia Nchi Kupitia Mifumo ya Ikolojia; Mradi wa Kusaidia Utekelezaji na Usimamizi wa Mbinu Jumuishi za Mazingira Katika Kuongoa na Kurejesha Ikolojia Iliyoharibika na Hifadhi ya Bioanuai; na Mradi wa Kusimamia Uhifadhi na Matumizi Endelevu ya Bonde la Ziwa Nyasa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Miradi mingine itakayotekelezwa na Ofisi katika mwaka 2019/20 ni pamoja na:- Mradi wa Kujenga Uwezo wa Taasisi Kusimamia na Kupunguza Athari za Mazingira kwa Jamii za Vijijini Katika Sehemu zenye Ukame; Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kutekeleza Sheria ya Mazingira; Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi Kupunguza Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozone; Mradi wa Kutekeleza Mpango wa Ufuatiliaji na Udhibiti wa Taka Zinazodumu Katika Mazingira Kwa Muda Mrefu; Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kitaasisi wa Kusimamia Kemikali na taka nchini; na Mradi wa Kuhuisha Uhusiano Kati ya Afya na Mazingira na Uwezo wa Kisheria na Kitaasisi Katika Udhibiti wa Kemikali na Taka.

 

HITIMISHO NA SHUKRANI

 1. Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni ya Muungano ambao una umuhimu wa pekee kwa Taifa na umekuwa ni utambulisho wa Taifa letu na kielelezo cha umoja wetu katika kudumisha Amani na Usalama wa nchi yetu. Mwaka huu Muungano wetu unatimiza miaka 55 tangu kuasisiwa kwake. Ninatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuuthamini, kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano ili jitihada za kusukuma mbele maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa faida za pande zote mbili.

 

 1. Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Muungano wetu unaendelea kuimarika na kushamiri. Chini ya uongozi wao hakuna changamoto yoyote inayoweza kutufarakanisha, kututenganisha wala kuturudisha nyuma. Katika mwaka 2019/20 Ofisi na Serikali kwa ujumla itaendelea kuyafanyia kazi mambo yote yanayoleta changamoto katika utekelezaji wa masuala yanayohusu Muungano na kutoa elimu kuhusu Muungano ili uendelee kuimarika.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mazingira katika mustakabali wetu na maendeleo ya uchumi wa viwanda, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa mazingira na maliasili za nchi yetu zinalindwa na kuhifadhiwa. Ninapenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Ofisi imejipanga kuipa elimu ya mazingira kipaumbele kwa jamii ili kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa. Aidha, Ofisi itahakikisha masuala yote yanayohusu uharibifu wa mazingira yanapatiwa ufumbuzi. Vilevile, Ofisi itaendelea kutoa miongozo ya hifadhi ya mazingira katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kuhifadhi mazingira kwa kuangalia mifumo ya ikolojia, mifumo ya uzalishaji mali, na mifumo ya uchumi ya matumizi ya rasilimali asili.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kuwashukuru walionisaidia kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi. Shukrani zangu za dhati na za kipekee ni kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake na dira na mwelekeo aliotupatia kuhusu majukumu yetu. Aidha, ninamshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake makini uliotuwezesha kutekeleza majukumu yetu. Ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, (Mb.), Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa ushirikiano anaonipa katika utekelezaji wa kazi za Ofisi. Vilevile, ninapenda kuwashukuru Mhandisi Joseph K. Malongo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais; Balozi Joseph E. Sokoine, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais; Ndugu Ali Mufuruki, Mwenyekiti wa Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Mazingira na Wajumbe wa Bodi ya Mfuko huo; Dkt.Samuel Mafwenga Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira; Wakuu wa Idara na Vitengo; na Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza kwa michango yao katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu. Pia ninawashukuru wale wote waliotuwezesha kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa kipindi kilichopita, na ambao wamesaidia katika kuandaa Mpango na Bajeti ya mwaka 2019/20.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ofisi imefanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo. Ninapenda kuwataja baadhi ya washirika wa maendeleo ambao Ofisi imefanya nao kazi kwa karibu kama ifuatavyo: Serikali ya Norway; Serikali ya Canada; Serikali ya Sweden; Serikali ya Italia; Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea; Umoja wa Nchi za Ulaya (European Union EU); Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (United Nations Development Programme – UNDP); Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization – UNESCO); Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP); Mfuko wa Mazingira wa Dunia (Global Environment Facility – GEF); Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma za Miradi (United Nations Office for Project Services – UNOPS); Benki ya Dunia (World Bank – WB); Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank – AfDB); Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (United Nations Industrial Development Organization – UNIDO); Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Denmark (Danish International Development Agency DANIDA); World Wide Fund for Nature – WWF; Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo (International Fund for Agricultural Development – IFAD); Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund – GCF); Shirika la Kilimo na Chakula Duniani ( Food and Agriculture Organization – FAO); Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (Gesellschaft fiir Internationale Zusammenarbeit – GiZ); Kikundi cha Washirika wa Maendeleo kinachoshughulikia Mazingira (Development Partners Group on Environment – DPGE); Asasi Zisizo za Kiserikali (AZISE); na Sekta binafsi. Aidha, ninapenda nitumie fursa hii kuwaomba washirika wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano katika kipindi kijacho ili tuweze kufanikiwa zaidi katika kulinda na kuimarisha Muungano wetu na kulinda na kuhifadhi mazingira yetu.

 

MAOMBI YA FEDHA

 1. Mheshimiwa Spika, ili Ofisi iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyopangwa, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liidhinishe maombi ya fedha kwa mwaka 2019/20, kama ifuatavyo:

 

Fungu 26: Makamu wa Rais

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe Makadirio ya Matumizi ya Sh. 7,855,093,000 fedha za Matumizi ya Kawaida kwa mwaka 2019/20. Kiasi hiki kinajumuisha fedha za Mishahara ya watumishi Sh. 1,120,128,000 na fedha za Matumizi Mengineyo Sh. 6,734,965,000.

 

Fungu 31: Ofisi ya Makamu wa Rais

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba Bunge lako Tukufu, liidhinishe makadirio ya matumizi ya Sh. 29,066,298,442 kwa Fungu hili. Kiasi hiki kinajumuisha Sh. 9,847,374,000 fedha za Matumizi ya Kawaida na Sh. 19,218,915,442 fedha za Miradi ya Maendeleo. Bajeti ya Matumizi ya Kawaida inajumuisha Sh.  2,759,365,000 fedha za Mishahara na Sh. 7,088,009,000 fedha za Matumizi Mengineyo. Fedha za Matumizi Mengineyo zinajumuisha Sh. 2,808,957,000 Ruzuku ya Mishahara ya watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira. Aidha, fedha za Miradi ya Maendeleo zinajumuisha Fedha za Ndani Sh. 1,000,000,000 na Fedha za Nje Sh. 18,218,915,442.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja.