MAKAMU WA RAIS AFANYA ZIARA SIHA NA HAI MKOANI KILIMANJARO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya tano imekusudia maendeleo na panapo hitajika maendeleo lazima ukweli usemwe.

Akihutubia wakazi wa kijiji cha Matabi wilayani Siha Makamu wa Rais alisema “Wakazi wa Siha hamna budi kubadilika mchague watu wenye itikadi ya maendeleo”

Makamu wa Rais ameendelea na ziara yake ambayo leo alikuwa katika wilaya ya Siha na Hai mkoani Kilimanjaro ambapo aliweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha pamoja na mambo mengine alihutubia wakazi wa kijiji cha Matabi.

Wananchi wa kijiji hicho walimueleza Makamu wa Rais tatizo la ukosefu wa ardhi ya makazi ambapo watu zaidi ya 11,000 hawana makazi.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema matatizo ya ardhi Siha yataisha kabla ya 2020.

Akiwa Wilayani Hai Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ufunguzi ya wodi ya Wanawake na kutembelea mradi wa shamba la maua ambapo pamoja na kujionea shughuli mbali mbali katika shamba hilo la muwekezaji wa kigeni Makamu wa Rais alizungumza na wafanyakazi wa hapo ambao walimueleza ugumu na changamoto wanazozipata.

Mwisho Makamu wa Rais alihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kwa Sadala ambapo alihimiza wakazi wa Hai kuchagua viongozi bora watakaoendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.

Makamu wa Rais aliambatana na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Wiliam Lukuvi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo.