MAKAMU WA RAIS AUTAKA MKOA WA MANYARA KUTUMIA SHERIA YA MAZINGIRA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameutaka Uongozi wa mkoa wa Manyara kutumia sheria za mazingira kulinda vyanzo vya maji.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo mjini Babati akiwa kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za kimaendeleo.

“Tumieni sheria ya mazingira inayotaka kuwe na mita 60, hii itasaidia kulinda na kutunza vyanzo vya maji, washirikisheni wataalam wa mazingira katika hili” alisema Makamu wa Rais.

Leo katika ziara yake wilayani Babati, Makamu wa Rais ametembelea kiwanda cha mbolea Minjingu, amezindua jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (BAWASA), kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa mtandao wa barabara Babati pamoja na kuhutubia wananchi wa Babati mjini katika uwanja mpira wa Kwaraa.

Katika hotuba yake kwa wakazi wa Babati mjini Makamu wa Rais amesema ziara yake ilianzia Mererani wilayani Simanjiro ambapo ameshuhudia ongezeko la ukusanyaji mapato pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya madini yetu.

Pia amesisitiza kwa wananchi kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kwani kufanya hivyo kutapunguza migogoro mingi haswa ya ardhi.

Makamu wa Rais ameziomba taasisi za maji katika mji wa Babati kuangali mpya tozo wanazowatoza wananchi kwani ni kubwa.

Kwa upande mwingine Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISENI Selemani Jafo amesema Serikali inajenga hospitali mpya 67 ndani ya mwaka mmoja, vituo vya afya 350 ndani ya miezi 18, shule za sekondari 89 kongwe zinafanyiwa ukarabati, kwa upande wa miundo mbinu zaidi ya kilomita 6 kati ya 10 za mtandao wa barabara Babati mjini zimekamilika.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Manyara ndugu Alexander Mnyeti amesema wamekuwa wakijitahidi kutatua migogoro mbali mbali hatua kwa hatua na wameweza kusimamia miradi kwa ubora unaotakiwa “Pesa za miradi zinaenda sehemu husika na hii ndio imetupa sifa ya kuwa mkoa wa pili Kitaifa katika mbio za mwenge za mwaka huu”.

Nae Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Mhe. Pauline Gekul pamoja na mambo mengine alikishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kumpokea na kumpa nafasi ya kukitumikia chama hicho kama Mbunge.