Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 3776654.NAIBU WAZIRI LUHAGA MPINA AKUTANA NA NEMC NA SUMATRA

 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, amepokea ripoti kutoka kwa uongozi wa Sumatra na Nemc ambao waliagizwa kufuatilia maagizo aliyoyatoa mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea bandari ya Dar es Salaam na kutoa maagizo kadhaa.

Bi. Blandina Cheche kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) amesema kuwa  Ofisi yake imepokea taarifa kutoka Mamlaka ya Bandari inayoonyesha aina na kiasi cha  taka kinachozaliwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari – Machi.

Taarifa hiyo inaonyesha pia kiasi cha taka zinazozalishwa na njia zinazotumika kuziteketeza. Bi. Blandina ameainisha kuwa ukaguzi maalumu kwa kutumia ndege umefanyika tarehe 20/22/ Januari, 10/11/ Februari na 15/17 Machi na kubaini kuwa hakuna uchafuzi uliobainika kufanywa na meli baharini katika kipindi husika. Aidha, imebainishwa kuwa jumla ya meli 79 za nje na 29 za ndani zimekaguliwa katika kipindi husika.

Kwa upande mwingine Meneja wa Leseni za usafiri barabarani Bw. Leo Ngowi kutoka Sumatra amesema kuwa Ofisi yake imeandaa mabango  (stikers) maalumu zinazotoa elimu kwa umma juu ya namna bora za matumizi ya Vyoo kwenye barabara kuu na kuhamasisha Halmashauri na watu binafsi kujenga Vyoo kwenye barabara kuu ili kuepusha uchafuzi wa mazingira.

Naibu Waziri Luhaga Mpina ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuitisha kikao cha wadau wakiwemo Nemc, Wizara ya Afya, Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kilimo, Mamlaka ya bandari pamoja na Sumatra ili kujadili namna bora ya usimamizi wa taka bandarini na katika vyombo vya usafiri nchi kavu.

Pia, amewaagiza Barala la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ndani ya miezi miwili kuandaa Muongozo utaoanisha namna bora ya kutupa taka. Muongozo huo pia utatumika katika bandari kubwa zote nchini na vivuko pia.

Taarifa iliyowasilishwa leo ni kutokana na maagizo aliyotoa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam tarehe 19/12/2016 baada ya malalamiko ya wananchi juu ya uchafuzi wa Bahari kutokana na umwagaji wa mafuta kutoka melini.


 

<< Back to News Archive.