Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 3784837.MHE. MAKAMBA AKUTANA NA VIONGOZI WA TAASISI ZA MUUNGANO

 Katika mwendelezo wa Ziara ya siku saba visiwani Zanzibar hii leo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amekutana na Viongozi wa Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar.

Waziri Makamba amesema kuwa, uwepo wa  taasisi za Muungano ni pamoja na uwepo wa Ofisi katika pande zote mbili za Muungano na kwa kiasi kikubwa Wizara na Taasisi zimeitikia wito wa kuwa na taasisi Zanzibar.

Katika kikao hicho baadhi ya viongozi hao wamesema kuwa kuna changamoto katika utendaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja uhaba wa watumishi kwa taasisi zilizopo Zanzibar, uzito na uwezo unazopewa taasisi hizo kwa upande wa Zanzibar, bajeti na vitendea kazi katika kutimiza majukumu yao.

Aidha, Waziri Makamba amesema kuwa dhamira ya Serikalini ni kuona changamoto tajwa zinapatiwa ufumbuzi mapema ikiwa ni pamoja na kuziwasilisha katika sekta/Wizara husika, na Ofisi ya Makamu wa Rais kama waratibu na wafuatiliaji wa mambo ya Muungano ameahidi kuwasilisha hoja hizo katika Vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Uwepo wa taasisi hizi ndio unakamilisha hasa kitu kinachoitwa Muungano kama ilivyoorodheshwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inapendeza kuona kwamba mambo haya yanafanyika kwa pande zote mbili kwa manufaa na ustawi wa Muungano wetu". Makamba alisisitiza

Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kufuatilia masuala yanayohusu taasisi za Muungano kwa upande wa Zanzibar kwa karibu kwa kushirikiana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha majukumu yote yanatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.

Waziri Makamba yuko Zanzibar katika ziara ya kikazi yenye Lengo la kuimarisha ushirikiano hasa kuangalia namna bora ya kushughulikia matatizo yaliyopo katika Muungano, kubadilishana uzoefu katika utendaji wa taasisi za Muungano na kuangalia namna bora ya kuboresha utendaji na utekelezaji wa masuala ya Muungano.

 


 

<< Back to News Archive.