Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 4012574.KAMATI YA BUNGE YAWASILI MKOANI IRINGA

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira hii leo imeendelea na ziara ya kazi kwa kupokea taarifa ya hali ya Mazingira Mkoani Iringa.

Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Kangi Lugola amesema kuwa  ni vema Kamati hiyo imetembelea Mkoa wa Iringa kwa  kuwa kuna changamoto kubwa ya kimazingira katika Mto Ruaha Mkuu na Ofisi yake iliunda kikosi kazi maalumu cha kunusuru mto huo.

“Naamini Kamati itaishauri Serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza usimamizi wa mazingira nchini, maana maendeleo yoyote kwa namna moja ama nyingine yanategemea hifadhi endelevu ya mazingira” Lugola asisitiza.

Akitoa taarifa ya Mkoa wa Iringa mbele ya Kamati hiyo ya Bunge, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza amesema kuwa Kamati hii ni muhimu sana kwa kuwa suala la Mazingira na Viwanda vinachangia katika ukuaji wa Uchumi kwa kuzingatia malengo ya Serikali ya kuwa na Uchumi wa Viwanda.

Aidha Bi. Masenza amesema kuwa katika Mkoa wake kampeni ya Upandaji miti kama ilivyoelekezwa na Serikali  inatekelezwa ipasavyo kwakuwa kila Wilaya imevuka lengo la kupanda miti Milioni Moja na Laki tano kila mwaka, na kupelekea Mkoa kuwa chanzo kikubwa cha upatikanaji wa mbao na nguzo za umeme.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Innocent Bashungwa ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kuwa mstari wa mbela katika kuhimiza suala la upandaji miti na kutoa wito kuwa kampeni hii ya upandaji miti kwa wingi ifanyike nchi nzima na kuitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mfuko wa Mazingira kusaidia rasilimali fedha kwa ajili ya kampeni hiyo.

Kamati inaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Iringa na hapo kesho itatembelea vyanzo mbali mbali vya maji vilivyohifadhiwa katika Wilaya ya Iringa Vijijini.


 

<< View list of News and Events.