Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 3777943.Mkutano wa Tano wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika

 

Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Mamlaka ya ziwa Tanganyika umefanyika mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya mkataba uliounda mamlaka hiyo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk. Terezya Huvisa amesema kuwa ili kulinusuru Ziwa Tanganyika jitahada za Nchi zote nne ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili ziwa hilo kwa sasa kwa kutumia fursa zilizopo.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira ikiwa ni pamoja na kujaa kwa taka za majumbani na zile za viwandani, uvuvi haramu kutokana na ongezeko la watu, kilimo na ufugaji usio endelevu. Hata hivyo Waziri Huvisa amewakumbusha wajumbe wa Mkutano huo kuwa Ziwa Tanganyika linaunganisha Nchi zote nne badala ya kuzitenganisha, hivyo ni muhimu kuwa na mikakati endelevu ya kuhifadhi ziwa hilo.

Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano huo ni pamoja na Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa ambao kwa sasa unafanya kazi katika nchi zote pamoja na Mkakati wa kukusanya fedha kwa ajili ya kuwa na usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika baadaya ya mwaka 2013 ambapo fedha za wafadhili zitafikia kikomo.

Katika Mkakati huo wa kukusanya fedha Nchi zote nne zimetia saini makubaliano ya kuchangia fedha ili hifadhi ya Ziwa hilo iwe endelevu, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

 

 

 

Mkutano huo umefanyika Tanzania kwa mara ya pili, mkutano mwingine kama huo ulifanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2007. Mamlaka hiyo ya Ziwa Tanganyika inaundwa na nchi za Zambia, Burundi, Congo (DRC) na mwenyeji Tanzania.

 

 

 


 

<< Back to News Archive.