Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 3777929.Semina elekezi ya Masheikh wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA)

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA SEMINA YA MASHEIKH WA BAKWATA

Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal amefungua semina elekezi kwa Masheikh wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA inayofanyika katika ukumbi wa VETA mjini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha wanawahimiza waumini wao kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika nchi nzima Agosti 26 mwaka huu na kusisitiza kuwa msingi wa zoezi hilo ni Utanzania na kamwe halisimami katika misingi ya rangi, dini, kabila ama eneo analotoka mtu.

Alisema sensa ya watu makazi inatoa fursa kwa serikali kujua idadi kamili ya wananchi wake na pia kupata takwimu zingine muhimu zitakazosaidia kuratibu mipango ya maendeleo katika nchi.

Hili ni zoezi linalomhusu kila Mtanzania kwa kuwa linalenga kurahisisha mipango ya maendeleo kwa Watanzania,” alisema Makamu wa Rais na kusisitiza “Msingi wa zoezi hili ni UTANZANIA na kamwe halisimami katika misingi ya rangi, dini, kabila ama eneo analotoka mtu,”.

Dkt. Bilal aliwaambia Masheikh hao kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kama ilivyopangwa. Alibainisha kuwa hivi sasa maandalizi yote yamekamilika, kinachosubiriwa ni siku hiyo ya Watanzania kuhesabiwa.

Katika dini yetu tunazo hadithi mbalimbali zinazohusu zoezi hili la sensa. Naamini ninyi Masheikh mnazo hadithi nyingi za mifano kuhusu suala hili nyakati za Mtume (S.A.W). Ni vema sasa mkafunua vitabu vyenu na kuwapa waumini wenu nukuu mbalimbali zinazowiana ili waelewe vema umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya Taifa na kwa maendeleo ya jamii yetu,” alisisitiza.

Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Waislamu umuhimu wa kujifunza namna bora ya kutumia benki zisizotoza riba za Kiislamu na kutumia benki hizo vizuri kwa kujipatia mikopo itakayowasaidia kuanzisha ya miradi ya kuwaondolea umaskini.

Aliwasisitiza wanazuoni watakaotoa mada hiyo kwenye semina hiyo kuhakikisha wanawaelimisha vyema washiriki hao kuhusu matumizi bora ya mikopo ya benki zisizo na riba katika kujikomboa na umasikini.

Alisitiza pia suala la utii wa sheria za nchi bila shuruti na uboreshaji elimu kwa kuanzisha shule ili kuwawezesha vijana kupata elimu na hatimaye waweze kumudu kuishi vema katika dunia ya sasa.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais

Dodoma

Julai 15, 2012

 


 

<< Back to News Archive.