Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
Total site visits: 3777790.MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI 5 JUNI, 2014

Tarehe 5 Juni, 2014 Watanzania tutaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya Mazingia Duniani.  Kama mnavyofahamu siku ya tarehe 5 Juni iliamuliwa kuwa  iwe Siku ya Mazingira Duniani kwa Azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, kama kielelezo cha ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira uliofanyika huko Stockholm, nchini Sweden.

Aidha, Azimio la kuunda chombo pekee cha Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme-UNEP, lilipitishwa siku hiyo. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha siku ya mazingira duniani kila mwaka, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa. Kimataifa, ujumbe wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni: “Chukua hatua kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” (Raise your Voice, Not the Sea Level). Kaulimbiu hii inahimiza kuwajibika kwa kila mtu katika kuhifadhi na kutunza Mazingira. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Kimataifa yataadhimishwa katika kisiwa cha Barbados, moja ya visiwa vya Karibeani. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho katika kisiwa cha Barbados yanatokana na ujumbe wa mwaka huu ambao unalenga kunusuru visiwa vinavyoathirika na Mabadiliko ya Tabianchi.
 
Hapa nchini  maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kitaifa mkoani Mwanza. Mkoa wa Mwanza umechaguliwa kutokana na changamoto za ukame unaoendelea katika mkoa huu na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na kilimo kisichokuwa endelevu kando kando ya Ziwa Victoria na uvuvi usioendelevu wa kutumia sumu na makokoro.

 -->

TAMKO LA MHESHIMIWA ENG. DKT. BINILITH S. MAHENGE (MB), WAZIRI WA NCHI - OFISI YA MAKAMU WA RAIS, KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI 5 JUNI, 2014

Ndugu wananchi,

Tarehe 5 Juni, 2014 Watanzania tutaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya Mazingia Duniani.  Kama mnavyofahamu siku ya tarehe 5 Juni iliamuliwa kuwa  iwe Siku ya Mazingira Duniani kwa Azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, kama kielelezo cha ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira uliofanyika huko Stockholm, nchini Sweden. 

Aidha, Azimio la kuunda chombo pekee cha Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nations Environment Programme-UNEP, lilipitishwa siku hiyo. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiadhimisha siku ya mazingira duniani kila mwaka, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa. Kimataifa, ujumbe wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni: “Chukua hatua kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” (Raise your Voice, Not the Sea Level). Kaulimbiu hii inahimiza kuwajibika kwa kila mtu katika kuhifadhi na kutunza Mazingira. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Kimataifa yataadhimishwa katika kisiwa cha Barbados, moja ya visiwa vya Karibeani. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho katika kisiwa cha Barbados yanatokana na ujumbe wa mwaka huu ambao unalenga kunusuru visiwa vinavyoathirika na Mabadiliko ya Tabianchi.  

Hapa nchini  maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kitaifa mkoani Mwanza. Mkoa wa Mwanza umechaguliwa kutokana na changamoto za ukame unaoendelea katika mkoa huu na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na kilimo kisichokuwa endelevu kando kando ya Ziwa Victoria na uvuvi usioendelevu wa kutumia sumu na makokoro. 

Ndugu wananchi,

Ujumbe wa mwaka huu kitaifa unahimiza wananchi wote Kutunza Mazingira ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Ujumbe huu unalenga kuelimisha na kuhamasisha wananchi vijijini na mijini kuhusu kukabiliana na masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi. Mabadiliko ya tabianchi ni mabadiliko ya kudumu katika mifumo ya hali ya hewa na uso wa dunia yanayotokana na ongezeko la gesijoto linalosababishwa na shughuli za maendeleo ya binadamu. Mabadiliko hayo hutokea baada ya kipindi kirefu, takriban zaidi ya miaka 30. Tatizo la ongezeko la mabadiliko ya tabianchi kutokana na ongezeko kubwa la uzalishaji wa gesi joto duniani (greenhouse gases-GHG) unasababishwa na shughuli za uzalishaji na matumizi yasiyoendelevu ya nishati viwandani, usafirishaji, shughuli za kilimo chenye matumizi makubwa ya mbolea hususan, katika nchi zilizoendelea, na   ukataji miti ovyo. Kwa kiwango kikubwa tatizo hili la Mabadiliko ya Tabianchi limechangiwa na shughuli hizi zinazofanyika katika nchi zilizoendelea.  Hata hivyo baadhi ya shughuli kama vile kilimo na ukataji wa misitu katika nchi zinazoendelea zimekuwa zikichangia pia.  Hivyo ujumbe wa mwaka huu unalenga katika kuwaelimisha wananchi juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwahimiza kukabiliana na athari hizo.  

Ndugu wananchi,

Tunaweza kutoa mchango wetu katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kudhibiti uchomaji moto wa misitu na uoto wa asili. Jitihada hizi zitasaidia pia katika kuongeza uwezo wetu wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Kitaifa ujumbe wa mwaka huu unasisitiza kwamba upandaji na utunzaji miti ni moja ya hatua muhimu za kuhifadhi mazingira hususan, kwenye vyanzo vya maji; kudhibiti uharibifu wa mazingira ya ardhi; kukabiliana na ukame na kuenea kwa hali ya jangwa; na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Ndugu wananchi,

Kwa mujibu wa taarifa ya Tano ya Chombo cha Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi,  Sekta ya Nishati inachangia (25.9%),  viwanda (19.4%) misitu (17.4%) usafirishaji (13.4%) sekta ya kilimo (13.1%), na sekta zingine (10.86%). Shughuli hizi ndizo chanzo cha ongezeko la gesijoto duniani. Hata hivyo, mchango wa nchi zinazoendelea bado ni kidogo sana. Natoa wito kwa  wananchi wote nchini kushiriki kikamilifu katika juhudi linazolenga kukabiliana na tatizo hili kwa kuwa nchi zinazoendelea ndizo zimekuwa waatharika wakubwa wa athari za Mabadiliko ya Tabianchi.  

Aidha, kwa kuzingatia mchango mkubwa wa nchi zilizoendelea katika tatizo la mabadiliko ya tabianchi, natoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za kupunguza gesijoto duniani na kusaidia nchi na wananchi katika nchi zinazoendelea kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.  

Ndugu wananchi,

Napenda kutoa wito Kila mkoa ujipange kufanya shughuli zinazolenga hifadhi ya mazingira. Aidha, tunapoadhimisha Wiki ya Mazingira Duniani tarehe 1 – 5 Juni tufanye yafuatayo :-

·        Kuchukua hatua za kudhibiti uchomaji moto ovyo katika maeneo ya vijijini na mijini

·        Kusafisha maeneo ikiwemo kuzoa taka, kuzibua mifereji ya maji machafu na kufukia madimbwi ya maji katika maeneo ya makazi;

·        kupanda miti inayofaa maeneo ya vyanzo vya maji;

·        Kusafisha visima na vyanzo vingine vya maji;

·        Kupanda nyasi na miti inayofaa palipo na mvua na maji ya kutosha;

·        Tuhamasishe matumizi ya vyoo bora;

·        Kilimo chetu kizingatie matumizi bora ya ardhi na matumizi ya mbolea isiyokuwa na athari kwa mazingira;

·        Wenye viwanda wazingatie matumizi bora ya uzalishaji wa bidhaa na kupunguza uzalishaji wa gesi joto;

·        Tuongeze matumizi ya nishati mbadala na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kuzingatia teknolojia yenye kutumia kiasi kidogo cha kuni na mkaa; na

·        Tuweke mazingira yetu kwa ujumla kuwa safi siku zote. 

Ndugu Wananchi;

Mwisho, napenda kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya uhamasishaji na ukuzaji wa weledi kwa wananchi hasa katika masuala ya mazingira.  Naomba vyombo hivi  viendeleze juhudi zao za kuuelimisha umma wa Watanzania kuhusiana na mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira. Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika hili na naamini vinaweza kusaidia sana. 

Nimalizie kwa kuwakumbusha kwamba hifadhi ya mazingira ni jukumu letu sote  na la kila siku  na isiwe kusubiri wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani tu.  Tunza Mazingira ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi” 

Ahsanteni sana

<< Back to News Archive.