Serikali kuendelea kuratibu miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Jimbo – Sima

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amesema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya majimbo ya uchaguzi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ufafanuzi huo umetolewa hii leo katika kipindi cha Maswali na Majibu wakati Mbunge wa Kiwani Mheshimiwa Abdalla Haji Ali alipouliza swali kwa Serikali sababu ambazo hupelekea fedha za mfuko huo kuchelewa kufika katika Majimbo ya Zanzibar.

Naibu Waziri Sima ameainisha utaratibu unaotumika katika mgawanyo wa fedha hizo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na jukumu la  Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kufanya mchanganuo wa kila Jimbo na kuwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ambayo huwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar ndiyo inayoingiza fedha kwenye akaunti za Majimbo ya Zanzibar.

“Hivyo, ni dhahiri kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha ucheleweshaji wa fedha hizo ukilinganisha na fedha zinazopelekwa kwenye Majimbo ya Tanzania Bara. Hata hivyo, jitihada za makusudi zinafanyika ili kuhakikisha fedha hizo zinaingia kwenye akaunti za Majimbo ya Zanzibar kwa wakati”. Sima alifafanua.

Mchanganuo wa mgawanyo wa fedha kwa kila Jimbo hutokana na vigezo vilivyoainishwa vya idadi ya watu katika Jimbo, ukubwa wa eneo na kiwango cha umaskini, uchambuzi ambao hufanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kuwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar kwa utekelezaji.

Kuanzia mwaka 2010, Ofisi ya Makamu wa Rais imeratibu na kufuatilia Miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa upande wa Zanzibar. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 16 ya Mwaka 2009 kwa lengo la kuchochea maendeleo ya majimbo ya uchaguzi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.