Balozi Seif: Kupatiwa eneo la kujenga Ofisi za SMZ Mjini Dodoma kutaimarisha Muungano

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi amesema kitendo cha Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kuipatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) eneo la ujenzi wa Ofisi zake Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma kitaendelea kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliodumu karibu Miaka 55.

Balozi Seif ametoa shukrani hizo wakati alipotembelea eneo lililokabidhiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Kujenga Ofisi zake katika eneo hilo eneo la Mahoma Makulu

Aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kuipatia eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 30 lililopo eneo la Mahoma Makulu ambapo alisema itafanya Serikali zote mbili kufanya Kazi kwa ukaribu zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais alisema kuwa wakati SMZ inatafakari namna ya kuanza ujenzi huo katika Bajeti ya mwaka ujao kuna haja kwa taasisi zilizokuwa tayari kuanza hatua za awali za ujenzi.

Aidha, alikipongeza Kikosi Kazi cha kuhamia Dodoma chenye Wajumbe kutoka pande zote Mbili za Tanzania Bara na Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoendelea kuisimamia katika kusanifu ujenzi wa Mji Mpya.

Aliuomba uongozi wa Kikosi Kazi hicho kutembelea Zanzibar na kuonana na viongozi pamoja na wananchi ili kutoa taaluma ya uelewa wa namna gani Mji Mpya wa Dodoma unavyotarajiwa kuwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema si vibaya kwa Kikosi Kazi hicho kuiga ujenzi wa Taasisi zilizoendelea katika upangaji wa Miji Mipya ya kisasa.