OFISI YA MAKAMU WA RAIS KUWA MFANO UTUNZAJI WA MAZINGIRA – MAKAMBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Muungano na Mazingira January Makamba  amesema Ofisi yake inatekeleza kwa vitendo maamuzi ya Serikali ya kuhamia Dodoma kwa kuanza na ujenzi wa jengo la utawala.

Hayo ameyasema leo mara baada ya kutembelea eneo la Mji wa Serikali ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais itajengwa. “Sisi kama watu wa mazingira lazima tuwe mfano, lazima tupande miti ya kutosha eneo lote hili liwe msitu” Makamba alisisitiza.

Waziri Makamba amesema kuwa kila mtumishi katika Ofisi yake atakabidhiwa miti ya kuitunza ili kuhakikisha eneo lote linakuwa na mandhari nzuri ya kuvutia.

Kwa upande mwingine Waziri Makamba amesema kuwa Ofisi yake ina dhamana ya kusimamia masuala ya Muungano na katika kuhakikisha hilo kiasi cha ekari kumi zimetengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kurahisisha masuala ya uratibu wa shughuli za Muungano.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais alieambatana na Waziri Makamba amesema kuwa awamu hii ya kwanza ya ujenzi itachukua ukubwa wa eneo mita za mraba 1050 na jengo litakuwa na Ofisi za viongozi waandamizi.

“Tunamalizia mazungumzo na Mkandarasi, tuweze kuanza ujenzi mapema iwezekanavyo na wiki ijayo tutaanza zoezi la kuzungusha nguzo kiwanja chote”