SERIKALI YAPATIA UFUMBUZI CHANGAMOTO MBALIMBALI ZA MUUNGANO

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais- imepatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Muungano. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mh. Mussa Sima,  wakati akijibu swali Bungeni la Mh. Fakharia Shomar Khamis (Mb). Lililouliza, Moja kati ya majukumu ya kuimarisha Muungano ni pamoja na kuhakikisha kuwa kero zote za Muungano zinatatuliwa; licha ya vikao vingi vilivyokaa na kujadili kero hizo: Je, ni kero ngapi tayari zimetatuliwa na zipi ambazo hadi sasa zimeshindikana kupatiwa ufumbuzi – Mh. Simma alisema kuwa Changamoto ambazo zimekwishapatiwa ufumbuzi ni 11 kati ya 15 zilizowasilishwa na kutafutiwa ufumbuzi .Changamoto 4 zilizobaki zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi na hakuna changamoto iliyoshindikana kupatiwa ufumbuzi.Aliongeza kuwa Dhamira ya Serikali  ni kumaliza changamoto zote zinazoukabili Muungano  ili uendelee kuwa nguzo pekee ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.

Akijibu swali la nyongeza la Mh. Fakharia Shomar Khamis Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mh. January Makamba linalohusu maandalizi na utaratibu wa vikao vya SMTna SMZ alisema kuwa ratiba na utaratibu wa vikao vya  kushughulikia changamoto za Muungano umeboreshwa hivyo kuna utaratibu mpya ambapo Kikao kikubwa  cha Makamu wa Rais ambacho ni cha Serikali zote mbili yaani Baraza la Mawaziri SMT na Baraza la Mawaziri SMZ kinakutana mara moja kwa mwaka,  kikao cha Mawaziri kinakutana mara moja kwa mwaka, Kikao cha Makatibu wakuu wote kinakutana mara mbili kwa mwaka na kikao cha Wataalamu wa Serikali zote kinakutan mara mbili kwa mwaka.

Aidha akijibu swali la Magdalena Sakaya, Matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini yamekuwa na athari kubwa kwenye uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa miji yetu:-Je, Serikali ina mikakati gani ya kuondoa matumizi ya plastiki  hapa nchini. Naibu Waziri  Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mh. Mussa Sima alisema kuwa: Ni kweli kuwa matumizi ya mifuko ya plastiki yameongezeka hasa kutokana na mifuko hii kutolewa bure kwenye maduka, masoko, migahawa na maeneo mbalimbali. Aidha, kutokana na baadhi ya nchi jirani kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kuruhusu uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ya nchi, kumekuwa na wimbi kubwa la uingizaji wa mifuko ya plastiki hapa nchini. Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeanza kuchukua hatua zifuatazo katika kuelekea kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki: kuhamasisha wajasiriamali, vikundi vya kinamama na vijana, sekta binafsi na viwanda kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala ikiwemo vikapu vya asili, mifuko ya karatasi na vitambaa.  Ofisi iliendesha mikutano miwili ya wadau katika mikoa ya Dar es Salaam (06 Novemba 2018) na Mwanza (18 Desemba 2018) kuelimisha umma kuhusu changamoto na athari za mifuko ya plastiki na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala kutokana na dhamira ya Serikali kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki katika siku zijazo.