TAMKO LA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA – SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI 2018

Tarehe 5 Juni, 2018 watanzania tutaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliamuliwa mwaka 1972, katika mji wa Stockholm nchini Sweden, kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira. Wakati wa mkutano huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nation Environment Programme, UNEP, lilipitishwa tarehe 5 Juni.  Tangu wakati huo, nchi mbalimbali zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, tarehe 5 Juni ya kila mwaka, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa. TAMKO LA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA), KWA VYOMBO VYA HABARI LITAKALOTOLEWA TAREHE 30 MEI, 2018

 Ndugu wananchi

Tarehe 5 Juni, 2018 watanzania tutaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliamuliwa mwaka 1972, katika mji wa Stockholm nchini Sweden, kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira. Wakati wa mkutano huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nation Environment Programme, UNEP, lilipitishwa tarehe 5 Juni.  Tangu wakati huo, nchi mbalimbali zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, tarehe 5 Juni ya kila mwaka, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.

Ndugu wananchi

Madhumuni ya maadhimisho haya ni kuelimisha jamii, masuala mabalimbali yahusuyo Mazingira, Kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maadhimisho haya, kuhamasisha jamii kuwa mstari wa mbele kuchukua hatua za kuhifadhi na kulinda mazingira ya maeneo yao, kutoa fursa kwa jamii mbalimbali kufahamu wajibu wao wa kuzuia madhara kwenye Mazingira yatokanayo na shughuli za kijamii wanazofanya, na  kuhamasisha jamii kuyafanya mazingira yao kuwa salama na masafi ili kila mtu afurahie hali hiyo katika maisha yetu ya sasa na ya vizazi vyinavyokuja.

 Ndugu wananchi

Kimataifa maadhimisho haya yanafanyika nchini India katika mji wa New Delhi. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Beat Plastic Pollution”. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kuepuka uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho haya nchini India ni kutokana na nchi ya India kuweka juhudi katika kupunguza uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki kwa kutumia mbadala wa plastiki na kurejeleza taka za plastiki. Aidha, India ni moja ya nchi zilizo mstari wa mbele katika kurejeleza taka za plastiki. UNEP imeamua India iwe mwenyeji wa maadhimisho haya kimataifa ili kutoa fursa kwa nchi nyingine kwenda India kujifunza kupunguza uchafunzi utokanao na plastiki na kurejeleza taka za plastiki.

Ndugu Wananchi

Hapa nchini maadhimisho ya Kitaifa yatafanyika Jijini Dar es Salaam. Serikali imeamua mkoa wa Dar es Slaam uwe mwenyeji wa Maadhimisho haya kwa lengo la kuwapa fursa wananchi wa jiji la Da re Salaam kuelimishwa na kuhamasishwa kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaolikumba jiji la Dar es Salaam, kama vile;- mafuriko; uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki; kubomoka kwa kuta za fukwe za bahari ya Hindi; pamoja na utumiaji wa kiasi kikubwa cha nishati ya mkaa. Ndugu Wananchi Uwepo wa matumizi makubwa ya mkaa hayapo tu katika Jiji la Dar es Salaam bali pia upo katika maeneo mengine ya nchi yetu. Hivyo basi kutokana na matumizi makubwa ya nishati ya mkaa katika nchi yetu, maadhimisho yetu ya kitaifa yataongozwa na Kaulimbiu inayosema; “Mkaa Gharama; Tumia Nishati Mbadala”. Serikali imeweka Kaulimbiu hii kutokana na kiasi kikubwa cha maeneo ya misitu yanayoharibiwa kwa ajili ya kupata mkaa. Takwimu zinaonyesha kwamba mpaka mwaka 2017 kiasi cha hekta 46,942 huharibiwa kila mwaka. Hapa nchini matumizi makubwa ya mkaa yako katika miji mkubwa ikiwemo Dar es Salaam, ambalo linatumia wastani wa tani 500,000 ya mkaa kila mwaka. Mahitaji haya yanaweza kuongezeka kadri jiji linavyoendelea kupanuka.

Ndugu wananchi

Kama mnavyofahamu uharibifu wa misitu unasababisha kuwepo kwa changamoto nyingine za mazingira kama vile ukame, majangwa, uharibifu wa ardhi, upotevu wa mimea asilia, upotevu wa viumbe hai mbalimbali upungufu wa upatikanaji wa maji na upungufu wa uzalishaji kwenye kilimo. Kutokana na changamoto hizo, wakati wa wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, kutakuwepo maonesho ya nishati mbadala wa mkaa na teknolojia zake. Maonesho haya yatafanyika katika viwanja vya mnazi mmoja tangu tarehe 31 Mei, hadi tarehe 5 Juni, 2018. Aidha, wajasiriamali na wataalam wa teknolojia ya nishati mbadala wa mkaa watatoa mafunzo kwa jamii na kuwahamasisha kutumia nishati mbadala wa mkaa. Tarehe 5 Juni, 2018 siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kutakuwa na utoaji wa zawadi kwa wadau watakaokuwa na teknolojia rahisi na endelevu ya kuzalisha nishati mbadala wa mkaa pamoja na wadau wanaoonyesha juhudi kubwa katika kuhifadhi mazingira kwa ujumla. Ninatoa wito kwa watanzania wote kwa ujumla kutumia fiursa ya maadhimisho haya kujifunza na kuhamasika kutengeneza na kutumia nishati mbadala wa mkaa ili kuweza kuokoa taifa letu na janga la  upotevu wa misitu.

Ndugu Wananchi

Kutokana na changamoto mbalimbali za mazingira zilizopo hapa nchini, maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na Kongamao la Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Uchumi litakalofanyika   tarehe 1 Juni, 2018 katika hoteli ya Hiyat Regency. Kongamano hilo litawahusisha wataalamu wa masuala ya Mazingira, Uchumi na Maendeleo pamoja na viongozi wa Serikali ambapo litajadili namna uchumi wa Tanzania unavyoathiriwa na Mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi.  

Ndugu Wananchi

Serikali pamoja na jamii nzima inatambua na kuheshimu nafasi ya viongozi wa dini katika jamii. Kwa kutambua hilo, serikali imeandaa Kongamano la viongozi wa madhehebu ya Dini mbalimbali litakalofanyika tarehe 2 Juni, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Kisenga Jengo la LAPF uliopo Kijitonyama. Viongozi hao watajadili nafasi ya Imani ya dini zao katika kuhifadhi mazingira. Tunaamini baada ya kongamano hilo wananchi wenye imani ya dini mbalimbali watahamasika kufanya juhudi katika kuhifadhi mazingira ya maeneo yao.

Ndugu Wananchi

Kwa kuwa maadhimisho ya kitaifa yatafanyika Jijini Dar es Salaam, ambako kuna changamoto nyingi za uharibifu wa mazingira yanayopelekea kudunisha usitawi wa jamii ya watu wanaoishi katika jiji hilo. Serikali imepanga pawepo na kongamano la wananchi wa Mkoa wa Jiji la Da res Salaam litakalofanyika tarehe 3 Juni, 2018 katika viwanja vya Zakhem Mbagala, ambapo wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanakaribishwa kuchangia mada mbalimbali zinazohusu changamoto za Mazingira katika jiji la Dar es Salaam.

Ndugu Wananchi

Jiji la Dar es Salaam pia linathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi, ambapo athari zake ni kuongezeka kwa mawimbi na ujazo wa bahari unaopelekea kubomoka kwa kingo za fukwe za bahari. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yalishaanza kuonekana kwenye kingo za ufukwe za bahari ya Hindi kando ya wa barabara ya Barack Obama maeneo ya Agakhani – Ocean road. Mwaka 2016 serikali kwa kushirikiana na wadau wa Mazingira duniani walishirikiana kujenga ukuta katika ufukwe wa bahari ya Hindi kando ya barabara ya Barack Obama. Tarehe 5 Juni, 2018 siku ya Kilele cha maadhimisho haya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafanya ufunguzi wa ukuta huo.

Ndugu wananchi

Nitoe wito kwa mikoa mingine yote kushirii kikamilifu katika maadhimisho haya kwenye mikoa yenu kwa kuhamasishana, kelimishana masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira. Aidha, nawahamsisha wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kushiriki kwenye shughuli zote za maadhimisho zinazofanyika wakati wa wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira, hususa kwenda kwenye viwanja vya mnazi mmoja kuona na kupata elimu juu ya matumizi ya nishati mbdala wa mkaa na teknolojia zake. Nitoe wito kwa wito kwa wajasiriamali wote kwenda kwenye viwanja vya mnazimmoja kujifunza namna ya kuingia kwenye ujasiriamali wa kutengeneza nishati mbadala wa mkaa tangu tarehe 31 Mei, hadi tarehe 5 Juni, 2018.

Mwisho, napenda kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya uhamasishaji na ukuzaji weledi kwa wananchi juu ya kaulimbiu ya kimataifa na kitaifa ya siku ya mazingira duniani mwaka huu. Naomba vyombo vya habari viendeleze juhudi hizi za kuelimisha umma kwamba kila mtu awe na mahusiano endelevu na mazingira na kupambana dhidi ya uharifu wa mazingira yetu. Tunatambua kwamba vyombo vya habari mna nafasi na uwezo mkubwa wa kuifikia jamii na naamini mnaweza kusaidia sana katika suala hili.

Nimalizie kwa kusisitiza kwamba, sote tuna jukumu la kuanza kubadilika kutoka kwenye matumizi ya mkaa na kuanza kutumia Nishati mbdala wa mkaa. Tukumbuke kwamba suala la hifadhi ya mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo.

 

Mungu Ibariki Tanzania

Ahsanteni Sana

JANUARY Y. MAKAMBA (MB.)

WAZIRI WA NCHI – MMZ