Kiswahili | English
Tafuta Tovuti hii kupitia hapa:
    
 
Total site visits: 3781157.Nafasi ya Makamu wa Rais Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tangu kuasisiwa kwa Muungano wetu mnamo tarehe 26 April, 1964, tumekuwa na viongozi wakuu nchini kutoka sehemu zote mbili za Muungano. Hati za Muungano zilitamka bayana kwamba kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wawili wa Rais ambao kati yao mmoja atatoka Zanzibar. Baada ya Muungano, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Makamu wa kwanza wa Rais alikuwa Sheikh Abeid Karume.

Aidha, tangu mwaka 1964 aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais alikuwa pia Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa pili wa Rais alikuwa pia Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Utaratibu huu uliendelea kwa takribani miaka thelasini na moja.

Karume Aboud Jumbe Ali Hassan Mwinyi
The late Sheikh Abeid Amani Karume  Mzee Aboud Jumbe  Mzee Ali Hassan Mwinyi

Hata hivyo, mnamo mwaka 1992, nchi yetu iliingia katika mageuzi makubwa ya mfumo wa kisiasa pale ilipoamua kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mabadiliko haya yalisababisha Katiba ya nchi ifanyiwe mabadiliko ili kuruhusu mfumo huu wa demokrasia ya vyama vingi ufanye kazi nchini ambapo nafasi mbalimbali za uongozi pia ziliguswa na mabadiliko hayo.

Mwaka 1994, kufuatia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kuruhusiwa nchini ilijitokeza haja ya kuifanyia mabadiliko nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili iweze kukidhi mageuzi haya ya kisiasa. Ilionekana kwamba katika mfumo huu mpya wa demokrasia ya vyama vingi si rahisi tena kuwa na Makamu wa Rais wawili kama ilivyokuwa wakati wa mfumo wa demokrasia ya chama kimoja.

Pia, ilibainika kwamba katika mfumo wa vyama vingi vya siasa upo uwezekano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar kutoka vyama tofauti vya siasa. Vile vile uwezekano utakuwepo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kutoka chama tofauti na kile cha Waziri Mkuu. Aidha, katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa itawezekana pia kwa Rais wa Zanzibar kutoka chama tofauti na kile anachotoka Waziri Kiongozi.

Katika mfumo huu ingewezekana pia kuwa na vyama tofauti vinavyotawala katika Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hali hii isingewezekana kama viongozi wakuu wanafuata muelekeo tofauti wa kiitikadi.

Kutokana na sababu hizo ilionekana ni vema Rais awe na Makamu kwa msingi kwamba viongozi hao watatoka sehemu tofauti za Muungano wetu. Aidha, ilionekana ni vema akawepo Makamu mmoja anayetoka chama kimoja cha siasa na Rais. Makamu huyo wa Rais atakuwa mgombea mwenza(running mate) wa Rais wake katika uchauzi mkuu wa kumchagua Rais.

Kwa mintaarafu hiyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ilifanyiwa marekebisho kupitia sheria na 34 ya mwaka 1994 na kuanzisha Ofisi ya Makamu wa Rais. Tangu kipindi hicho Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa na nafasi moja tu ya Makamu wa Rais.

Viongozi walioshika nafasi ya Makamu wa Rais tangu mkwaka 1964

 1. Hayati Sheikh Abeid Amani Karume  -  Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1964 – 1972
 2. Mzee Aboud Jumbe – Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1972 - 1984
 3. Mzee Ali Hassan Mwinyi – Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1984
 4. Hayati Mzee Idriss Abdul Wakil -  Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1985 – 1990
 5. Dr. Salmin Amour - Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1990 - 1995
 6. Mzee Rashid Mfaume Kawawa – Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1972 - 1977
 7. Hayati Edward Moringe Sokoine -  Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977– 1980/ 1983 – 1984
 8. Dr. Salim Ahmed Salim – Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1984- 1985
 9. Jaji Joseph Sinde Warioba – Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1985 - 1990
 10. Mzee Cleopa David Msuya- Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1980 – 1983/  Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1994 - 1995
 11. Mzee John Samwel Malecela – Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1990 - 1994