ZIARA YA MAKAMU WA RAIS WILAYANI HANANG

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kuhakikisha wakulima wanayafikisha mazao sokoni moja kwa moja bila kuwa na madalali wa mazao.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akihutubia wanachi kwenye uwanja wa wa shule ya msingi Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara.

“Tumejenga soko ili mkulima apate bei nzuri ya mazao yake, mazao ya mkulima yasogezwe sokoni mnunuaji kama ni Mtanzania au kama ni wa Nje anunulie pale sokoni” alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais ameendelea na ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za kimaendeleo wilayani Hanang.

Baadhi ya Shughuli ambazo Makamu wa Rais amefanya leo ni kutembelea mradi wa ujenzi wa Soko na Ghala Endagaw, kuweka jiwe la msingi la bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya Nangwa Sekondari ambapo aliendesha harambee na kuwezesha kupatikana kwa zaidi ya milioni 12, kuweka jiwe la msingi mradi wa maji Bassotu pamoja na kuzungumza na wananchi wa Katesh.

Aidha Makamu wa Rais aliwataarifu wananchi hao kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani mwaka 2019 kwa kuwataka wachague viongozi waadilifu, wazalendo na wachapa kazi.

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Rais alimjulia hali na kumpa pole Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Frederick Sumaye ambaye alifiwa na mama mzazi tarehe 7 Novemba 2018.

Makamu wa Rais alifika kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Sumaye na kusaini kitabu cha maombelezo.